Jeshi la Israel limeripoti kuwa Iran imefanya mashambulizi yaliyohusisha msururu wa makombora Ijumaa mchana. Ni wakati waziri wa mambo ya nje wa Iran akiwa mjini Geneva kwa mazungumzo katika juhudi za kuutatua mzozo huo.

Taarifa ya jeshi la Israel imesema ving’ora vya tahadhari vilisikika katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo baada ya Iran kuifyatulia makombora. Katika taarifa za awali kuhusu shambulio hilo, shirika la huduma za uokoaji la Magen David Adom la Israel limeripoti kuwa watu wawili wamejeruhiwa lakini halikutaja eneo la tukio.

Hayo yanajiri wakati Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Abbas Araghchi akifanya mazungumzo na wenzake wa Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Umoja wa Ulaya mjini Geneva katika juhudi za kutafuta suluhisho la kidiplomasia ili kuumaliza mzozo.