VIONGOZI wa nchi wanachama wa Jumuiya ya kijeshi ya NATO wameidhinisha rasmi ongezeko la asilimia tano ya Pato la Taifa kwa ajili ya matumizi ya ulinzi kwenye mkutano wao wa kilele uliofanyika mjini The Hague, Uholanzi.

Nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO zimekubaliana kuongeza kwa kiasi kikubwa matumizi yao ya ulinzi ili kumridhisha Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye aliisifu hatua hiyo kama “ushindi mkubwa” kwa Marekani — na kusisitiza ahadi ya nchi yake ya kuwalinda washirika wake wa Ulaya.

Trump alifurahi baada ya nchi 32 za NATO kukubaliana na lengo lake la asilimia tano ya pato jumla la taifa katika matumizi ya ulinzi kufuatia siku mbili za mazungumzo huko mjini The Hague nchini Uholanzi.

Trump pia alitia saini tamko la mwisho la kuthibitisha kujitolea kwa dhati kwa ahadi ya pamoja ya ulinzi wa NATO kwamba shambulio dhidi ya nchi moja mwanachama ni shambulio la wote – hatua ya kutia moyo kwa nchi za Ulaya zinazoihofia Urusi.

Kiongozi huyo wa Marekani alipendekeza mara kwa mara kwamba Marekani inaweza kuzuia ulinzi kutoka kwa nchi za Ulaya ambazo hazitaki kutumia fedha zaidi katika masuala ya ulinzi.