Na Mwandishi wetu

Wakati Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega na mkewe Mariam Abdallah Ibrahim wakiwa wamechukua fomu ya kuomba kuwania ubunge wa jimbo na viti maalum katika Mkoa wa Pwani, wadau mbalimbali wamehoji hatua hiyo imelenga kutatua kero za wananchi au ni ubinafsi wa madaraka.

Hatua hiyo imekuja baada ya Ulega kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kwa ajili ya kuwania Ubunge katika jimbo la Mkuranga, huku mkewe Mariam Ulega akiomba ridhaa ya chama hicho kwa kupitia viti maalum mkoa wa Pwani.

Ingawa walichukua fomu kwa nyakati tofauti ambapo Mariamu alichukulia katika ngazi ya Mkoa huku Ulega akichukua fomu hiyo katika ofisi za Chama Wilaya ya Mkuranga, baadhi ya wadau wamehoji kama wana dhamira ya kuwasaidia wananchi kwanini wasiache nafasi moja iende kwa mtu mwingine atakayekuwa na mawazo yasiyolingana kama ambavyo mume na mke wanaweza kuwa nayo.

Akizungumzia tukio hilo Athuman Sharifu Mkazi wa Mwandege, amesema mazingira ya kurundika mamlaka yote ya kuwaletea maendeleo wananchi hayapaswi kurundikwa katika mbawa za watu wenye Mawazo ya kulingana.

“Unadhani mke na mume wanaweza kuwa na mawazo tofauti juu ya maendeleo?..hilo haliwezekani mimi sijasoma lakini ninaamini ili uwe na maaendeleo ni lazima kila mmoja afikiripeke yake na atoe mawazo yake akiwa huru tofauti na mke na muwe wanavyoweza kuamua.

Alitolea mfano baadhi ya mambo yanavyokwama katika Serikali ya Uganda baada ya Rais kumteua mkewe kuwa Waziri wa Ulinzi na kusema kwa vyovyote watu hao hushauriana chumbani kabla ya kutoka nje na hakuna anayeweza kumkosoa mwenzie kuwa anakosea,hali aliyoeleza kuwa inaweza kutokea hata katika jimbo la Mkuranga ikiwa wahusika watapata madaraka wanayoomba.