*Takwimu zawaonyesha ambao kwa miaka mitano hawajawahi kuzungumza lolote bungeni

*Yaani hawakutoa hoja, kuchangia hoja, kuuliza swali la msingi wala kuuliza swali la nyongeza

Na Dennsi Luambano , JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wakati wabunge wakijipambanua kuwa ni wawakilishi wa wananchi bungeni, imefahamika kuwapo kwa baadhi yao ambao hawakutoa mchango wowote katika uhai wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; JAMHURI linaripoti.

Kipindi cha uhai wa Bunge la 12 kilianza Novemba 13, 2020 baada ya Rais Dk. John Magufuli kulizindua huku Spika akiwa ni Job Ndugai, na sasa Rais Samia Suluhu Hassan amesema litavunjwa rasmi Agosti 3, mwaka huu.

Wiki iliyopita Rais Samia alitoa hotuba ya kusitishwa kwa shughuli za Bunge likiwa chini ya Spika Dk. Tulia Ackson.

Wakati kukiwapo idadi ya kutosha ya wabunge ‘mabubu’ au waliozungumza mara moja tu bungeni, kwa upande mwingine wapo ‘wazungumzaji wazuri’ waliotoa michango au hoja zaidi ya mara 80 na kuuliza maswali zaidi ya mara 120.

Ndani ya miaka mitano ya uhai wa Bunge la 12, mikutano 19 imefanyika.

Taratibu za uendeshaji wa Bunge zinamtaka mbunge kuwasilisha maswali kwa njia ya maandishi ofisini kwa Katibu wa Bunge, yachambuliwe na kupelekwa wizara husika itakayotoa majibu kwenye vikao vya Bunge.

Mbunge pia hupata nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza baada ya majibu ya swali la msingi kutolewa na wizara husika.

Wakati hoja za serikali au bajeti zinapowasilishwa na kujadiliwa, mbunge huwa na fursa ya kuchangia kwa dakika 10 zinazoweza kupungua kutokana na idadi ya wachangiaji siku hiyo.

Takwimu hizi hapa

Tovuti rasmi ya Bunge inayo orodha ya wabunge wanaoongoza kwa kutochangia chochote kwa miaka mitano.

Miongoni mwao ni Mbunge wa Tunguu (CCM), Khalifa Salum Suleiman, ambaye hajawahi kuchangia wala kuuliza swali la msingi au la nyongeza, sawa na Mbunge wa Mfenesini (CCM), Zubeida Khamis Shaib.

Mbunge wa Mfenesini (CCM), Zubeida Khamis Shaib.

Wengine katika orodha hiyo ni Mbunge wa Wawi (CCM), Khamis Kassim Ali; Mbunge wa Mtambile (CUF), Seif Salim Seif na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Idd Mabrouk; huku Mbunge wa Chambani (CCM), Mohamed Abdulrahman Mwinyi akiuliza maswali ya msingi manne na ya nyongeza manne.

Katika orodha hiyo yupo pia Mbunge wa Monduli (CCM), Fredrick Lowassa, ambaye hajawahi kuchangia hoja, akiuliza swali moja la msingi na moja la nyongeza kwa miaka mitano.

Orodha hiyo inawataja Mbunge wa Amani (CCM), Abdul Yussuf Maalim, kuwa naye hajawahi kuchangia ila ameuliza maswali mawili ya msingi na sita ya nyongeza.

Mbunge wa Kijini (CCM), Yahya Ali Khamis, hajawahi kuuliza swali la msingi wala la nyongeza ila amechangia mara moja tu.

Mbunge wa Kwahani, Khamis Yussuf Mussa, hajawahi kuchangia ila ameuliza mara moja swali la msingi na moja la nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zulfa Mmaka Omar, amechangia mara mbili na hajawahi kuuliza swali la msingi wala la nyongeza.

Mbunge wa Tunguu (CCM), Khalifa Salum Suleiman

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Wanu Hafidh Ameir, amechangia mara moja, ameuliza swali la msingi moja na la nyongeza moja.

Orodha ya wabunge wenye michango michache bungeni inawajumuisha pia Mbunge wa Fuoni, Abbas Ali Mwinyi; Mbunge wa Mkwajuni (CCM), Khamis Ali Vuai; Mbunge wa Paje, Jaffar Sanya Jussa na Mbunge wa Bumbwini (CCM), Mbarouk Juma Khatib na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Bakar Yussuf.

Mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustine Holle, ametoa michango mara 27, ameuliza maswali tisa ya msingi na maswali saba ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Lucy Mayenga, amechangia mara 20 na ameuliza maswali ya nyongeza mara 21.

Mbunge wa Same Magharibi (CCM), Dk. David Mathayo, amechangia mara tano, ameuliza maswali 31 ya msingi na maswali 39 ya nyongeza na amemuuliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, swali moja katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo bungeni.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Josephine Chagulla, amechangia bungeni mara nne, ameuliza maswali 11 ya msingi na maswali 11 ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Khadija Hassan Aboud, amechangia mara 66, ameuliza maswali mawili ya msingi na maswali saba ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu, Maida Hamad Abdallah, amechangia mara 11, ameuliza maswali 14 ya msingi na 15 ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mariamu Mzuzuri, amechangia mara 18, ameuliza maswali mawili ya msingi na matano ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Munira Mustafa Khatib, amechangia mara 11, ameuliza maswali tisa ya msingi na 18 ya nyongeza.

Mbunge wa Morogoro Mjini (CCM), Abdulaziz Abood, amechangia mara nne, ameuliza maswali sita ya msingi na 10 ya nyongeza na kumuuliza Majaliwa swali moja.

Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, amechangia bungeni mara 31, ameuliza maswali mawili ya msingi.

Mbunge wa Kwimba (CCM), Mansoor Jamal, amechangia mara tisa na kuuliza swali moja la msingi.

Mbunge wa Sumbawanga Mjini (CCM), Aeshi Hilaly, amechangia mara 21 na kuuliza swali moja la msingi.

Mbunge wa Ole (CCM), Juma Hamad Omar, amechangia mara nane, ameuliza maswali mawili ya msingi na moja la nyongeza.

Mbunge wa Kahama Mjini (CCM), Jumanne Kishimba, amechangia mara 37, ameuliza maswali mawili ya msingi na moja la nyongeza.

Mbunge wa Bububu (CCM), Mwantakaje Haji Juma, amechangia mara tatu, ameuliza maswali 13 ya msingi na 12 ya nyongeza.

Mbunge wa Ziwani (CCM), Ahmed Juma Ngwali, amechangia mara 15, ameuliza maswali mawili ya msingi na matatu ya nyongeza.

Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Shamsi Vuai Nahodha, amechangia mara 24 na kuuliza swali moja la msingi.

Mbunge wa Chwaka (CCM), Haji Makame Mlenge, amechangia mara nane, ameuliza maswali saba ya msingi na saba ya nyongeza.

Mbunge wa Mtoni (CCM), Abdulhafar Idrissa Juma, amechangia mara 12, ameuliza maswali ya msingi mara tano na tisa ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Latifa Khamis Juwakali, amechangia mara tano, ameuliza maswali ya msingi mara 16 na 11 ya nyongeza.

Mbunge wa Handeni Vijijini (CCM), John Sallu, amechangia mara saba, maswali ya msingi ameuliza mara nane na tisa ya nyongeza.

Mbunge wa Gando (CCM), Salim Mussa Omar, amechangia mara nne, ameuliza maswali 10 ya msingi, matano ya nyongeza na moja kwa Majaliwa.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Rose Busiga, amechangia mara sita, ameuliza maswali manne ya msingi na tisa ya nyongeza.

Mbunge wa Kiwani (CCM), Rashid Abdalla Rashid, amechangia mara nane, ameuliza maswali matano ya msingi na saba ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Martha Gwau, amechangia mara saba, ameuliza sita ya msingi, 10 ya nyongeza na moja kwa Majaliwa.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk. Paulina Nahato, amechangia mara 17, ameuliza maswali ya msingi mara nne na tisa ya nyongeza.

Mbunge wa Ulanga, Salim Hasham, amechangia mara saba, ameuliza maswali 11 ya msingi na tisa ya nyongeza.

Mbunge wa Makunduchi, Haji Amour Haji, amechangia mara 16, ameuliza maswali matano ya msingi na matano ya nyongeza.

Mbunge wa Micheweni (CCM), Abdi Hija Mkasha, amechangia mara mbili, ameuliza maswali ya msingi mara nne na matano ya nyongeza.

Mbunge wa Mwanakwerekwe (CCM), Kassim Hassan Haji, amechangia bungeni mara mbili, ameuliza mara sita maswali ya msingi na mengine sita ya nyongeza.

Mbunge wa Magomeni (CCM), Mwanakhamis Kassim Said, amechangia mara 10, ameuliza mara sita maswali ya msingi na mara nne ya nyongeza.

Mbunge wa Nungwi (CCM), Simai Hassan Sadiki, amechangia mara 18, ameuliza maswali sita ya msingi na 12 ya nyongeza.

Mbunge wa Dimani (CCM), Mustafa Mwinyikondo Rajab, ameuliza maswali ya msingi mara tatu na moja la nyongeza.

Mbunge wa Shaurimoyo (CCM), Ali Juma Mohamed, amechangia mara tatu, ameuliza sita ya msingi na saba ya nyongeza.

Mbunge wa Morogoro Kusini Masahariki, Shabani Taletale, amechangia mara 10, ameuliza mara tano maswali ya msingi na 23 ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Aleksia Kamguna, amechangia mara tano, ameuliza mara tisa maswali ya msingi, nyongeza mara 19 na swali moja kwa Majaliwa.

Mbunge wa Mahonda (CCM), Abdullah Ali Mwinyi, amechangia mara 18, ameuliza mara tatu maswali ya msingi na mara moja la nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Juliana Masaburi, amechangia mara nne, ameuliza maswali matano ya msingi na matano ya nyongeza.

Mbunge wa Mpendae (CCM), Toufiq Salim Turky, amechangia mara nane na hajawahi kuuliza swali la msingi wala la nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Ali Mzee, amechangia mara tatu, ameuliza maswali saba ya msingi kisha nane ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Asya Sharif Omar, amechangia mara tano, ameuliza maswali tisa ya msingi na 10 ya nyongeza.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Assa Makanika, amechangia mara 10, ameuliza maswali saba ya msingi, tisa ya nyongeza na moja kwa Majaliwa.

Mbunge wa Pandani (CUF), Maryam Omar Said, amechangia mara 10, ameuliza mara tatu maswali ya nyongeza.

Mbunge wa Chonga (ACT), Salum Mohammed Shaafi, amechangia mara sita, ameuliza mara moja swali la msingi na la nyongeza mara moja.

Mbunge wa Makunduchi, Ravia Idarus Faina, amechangia mara tano, ameuliza mara mbili maswali ya msingi na mara tatu ya nyongeza.

Mbunge wa Welezo (CCM), Maulid Saleh Ali, amechangia mara tatu, ameuliza mara tano maswali ya msingi na manne ya nyongeza.

Mbunge wa Kiembesamaki (CCM), Mohammed Maulid Ali, amechangia mara tatu, ameuliza mara tatu maswali ya msingi na mara mbili ya nyongeza.

Mbunge wa Malindi (CCM), Mohamed Suleiman Omar, amechangia mara moja, ameuliza mara nne maswali ya msingi na matatu ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Hassan, amechangia mara 10, ameuliza maswali matano ya msingi na tisa ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Saada Mansour Hussein, amechangia mara saba, ameuliza mara mbili maswali ya msingi na mawili ya nyongeza.

Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Dk. Bashiru Kakurwa, amechangia mara tano na hajawahi kuuliza swali la msingi wala la nyongeza.

Mbunge Kutoka Baraza la Wawakilishi (CCM), Suleiman Haroub Suleiman, amechangia mara nne, ameuliza maswali manne ya msingi na manne ya nyongeza.

Mbunge Kutoka Baraza la Wawakilishi (CCM), Mwantatu Mbarak Khamis, amechangia mara tatu, ameuliza maswali ya msingi mara sita na sita ya nyongeza.

Mbunge Kutoka Baraza la Wawakilishi (CCM), Bahati Khamis Kombo, amechangia mara saba, ameuliza maswali ya msingi mara nne na manne ya nyongeza.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Aziza Sleyum Ally, amechangia mara moja, ameuliza maswali ya msingi mara tatu na matano ya nyongeza.