Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilwa

Mhasibu Mkuu Mkoa wa Tanga, Ahmed Bongi amejitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania kuteuliwa nafasi ya Ubunge Jimbo la Kilwa Kusini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Bongi ambaye alikuwa Mhasibu Mkuu Mkoa wa Lindi kabla ya kuhamishiwa mkoani Tanga amechukua fomu hiyo jana katika ofisi za CCM Kilwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Kilwa, Suraiya Kangusu .

Hii ni mara ya pili kwa mhasibu huyo kugombea nafasi hiyo ambako mwaka 2020 akiwa Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Lindi aliongoza katika mchujo huo na kushika nafasi ya kwanza. Hata hivyo, jina lake lilikatwa na vikao vya juu vya uamuzi wa chama na mbunge wa sasa ambaye alishika nafasi ya tatu kupewa nafasi.

Mwaka mmoja baadaye Bongi aliteuliwa kuwa Katibu Tawala ( DAS), wilayani Ruangwa kabla kurejeshwa katika kazi yake ya awali ya Uhasibu kisha kuhamishiwa mkoani Tanga kuwa Mhasibu Mkuu wa Mkoa ambako amehudumu kwa miaka mitatu sasa

Akizungumza mara baada ya kuchukua na kurejesha fomu hiyo , Bongi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Kilwa na na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa , amesema ameamua kugombea nafasi hiyo ili kuwatumikia zaidi wananchi na kutoa mchango wake kwa jamii.