Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Moshi

Zaidi ya wakazi 230,784 wa kata tisa katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, wameondokana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Karanga Darajani uliogharimu Sh2.4 bilioni.

Mradi huo ambao umeotekelezwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa), umezinduliwa jana Juni 28, 2025, na Mbio za Mwenge wa Uhuru.

Kukamilika kwa mradi huo, kumeongeza upatikanaji wa maji hadi kufikia saa 23.7 kwa siku na kuongeza uzalishaji kwa mita za ujazo 3,888 kwa siku.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa MUWSA, Mhandisi Kija Limbe amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Machi 1, 2023 na sasa umekamilika kwa asilimia 100, ukiwa umetumia fedha za ndani na wataalamu wa ndani ya mamlaka hiyo.

“Awali Muwsa hapa Manispaa ya Moshi ilikuwa inazalisha mita za ujazo 43,322 kwa siku, sawa na asilimia 60 ya mahitaji ya mita za ujazo 73,246. Mradi huu umeleta ongezeko muhimu na kupunguza upungufu wa maji ambao ulikuwa unafikia mita za ujazo 17,593 kwa siku,” amesema Limbe.

Ameongeza kuwa mradi huo umelenga kuboresha upatikanaji wa maji katika kata za Mawenzi, Bondeni, Pasua, Mabogini, Bomambuzi, Majengo, Kiboroloni, Msaranga pamoja na kata ya Mabogini.

Akizungumza kuhusu mradi huo,kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi amesema, “ Taasisi hii ya Muwsa ndiyo ina jukumu la kutekeleza ahadi ya Rais ya kuhakikisha maeneo yote ya Manispaa ya Moshi yapata maji safi na salama.Ni faraja kuona wananchi wa Moshi sasa wamepata huduma hii muhimu.”

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mzava amesema mradi umetumia chemchemi iliyolindwa kwa ukuta maalumu kuzuia maji ya mto kuingia, huku akieleza kuridhishwa na ushiriki wa wataalamu wa ndani katika utekelezaji wake.

Mkazi wa Mabogini, Rukaiya Saleheamesema mradi huo umepunguza adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji. “Kwa sasa tunaishi kwa amani bila kuhangaika,” amesema.

Mradi huo unajumuisha chemba nne, chemba kuu moja,mtaro wa kuzuia maji ya mvua,ukuta wa kinga,bomba la inchi 10 lenye urefu wa kilomita 2.3,pamoja na ofisi ya mitambo,pampu na umeme.Hadi sasa,wateja wapya 540 wameunganishwa na kazi ya uunganishaji inaendelea.

Mwenge wa Uhuru umepokelewa jana Juni 28, 2025, katika uwanja wa Ndege wa Moshi (Moshi Airport) ukitokea Kaskazini Pemba, Zanzibar na unatarajiwa kukimbizwa katika halmashauri zote saba za mkoa wa Kilimanjaro kuanzia leo hadi Julai 4, 2025.

Katika Mkoa wa Kilimanjaro, Mwenge utapitia miradi 52 yenye thamani ya Sh84.9 bilioni ambapo kati ya miradi hiyo, 23 itazinduliwa, 20 itawekwa mawe ya msingi na tisa itakaguliwa kabla ya kukabidhiwa mkoa wa Arusha Julai 5.