Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeutumia vyema msimu wa Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kama jukwaa la kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu haki za binadamu, wajibu wao wa kisheria, na umuhimu wa uchaguzi huru na wa haki nchini.
Akizungumza katika banda la Tume hiyo ndani ya maonyesho hayo yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere, Kamishna Mkazi wa Tume Zanzibar, Khatib Mwinyichande, alisema Sabasaba ni fursa muhimu ya kuwa karibu na wananchi, kupokea malalamiko yao, na kuwaelimisha kuhusu haki zao za msingi.
“Maonyesho haya yanatupa nafasi ya kukutana moja kwa moja na wananchi. Tunalinda haki zao, tunawaelimisha kuhusu wajibu wao, na tunawakumbusha kuwa hakuna mtu anayepaswa kunyimwa haki yake kwa misingi yoyote,” alisema Kamishna Mwinyichande.
Aidha, alieleza kuwa Tume hiyo, kama chombo huru cha kikatiba, ina wajibu wa kuhakikisha uchaguzi mkuu nchini unakuwa huru, wa haki na unaozingatia misingi ya utawala bora.
“Uchaguzi si tukio la kisiasa tu, bali ni haki ya msingi kwa wananchi. Tume yetu ina jukumu la kuhakikisha kuwa mchakato wote wa uchaguzi unazingatia sheria, haki za binadamu na misingi ya demokrasia,” alibainisha.
Mwinyichande alisema Tume itakuwa miongoni mwa waangalizi wa uchaguzi mkuu, kuanzia kampeni hadi upigaji kura, na itakuwa ikifuatilia mwenendo wa uchaguzi ili kubaini changamoto na mapungufu yanayoweza kuathiri haki za wananchi, kisha kuwasilisha ripoti kwa mamlaka husika kwa ajili ya maboresho ya baadaye.
Alisisitiza kuwa kazi ya Tume si tu kulinda haki baada ya matatizo kutokea, bali pia ni kuzuia ukiukwaji wa haki kabla haujatokea kwa njia ya elimu na ushawishi wa sera zenye mwelekeo wa haki na usawa.
Kwa ujumla, ushiriki wa Tume ya Haki za Binadamu katika Sabasaba mwaka huu umeonesha namna taasisi za umma zinavyoweza kutumia majukwaa ya kijamii kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu haki zao, wajibu wao, na njia salama za kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi kupitia uchaguzi wa kidemokrasia.
