Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia Dar es Salaam
TUME ya Ushindani (FCC) imewataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kulinda afya na usalama wao kwa kujiepusha na bidhaa bandia, huku ikisisitiza umuhimu wa elimu kwa jamii kuhusu haki za walaji na mazingira salama ya biashara.
Kauli hiyo ilitolewa Julai 4, 2025 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Hadija Ngasongwa, alipotembelea Banda la Viwanda na Biashara katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
“FCC haishughulikii tu makampuni au wawekezaji, bali inalinda afya ya jamii nzima. Tuna jukumu la kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa salama, bora na zinazokidhi viwango vya kisheria,” alisema Hadija.

Alibainisha kuwa moja ya changamoto kubwa kwa jamii ni upatikanaji wa bidhaa bandia, ambazo zinaweza kuleta madhara ya kiafya, kiuchumi na kijamii. “Elimu ni silaha kuu. Tunawahimiza wananchi kufika kwenye banda letu kujifunza namna ya kuzitambua bidhaa bandia,” aliongeza.
Hadija alisema FCC imekuwa ikitoa elimu kwa walaji kuhusu haki zao, ikiwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya manunuzi, kudai stakabadhi, na kuripoti bidhaa zisizo salama.
Pia aliwahamasisha wananchi wa kipato cha chini kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia maonyesho ya Sabasaba kwa kushirikiana na kampuni mbalimbali ili kukuza biashara zao kwa njia halali.

“Tunataka jamii ielewe kuwa kulinda haki ya mteja ni kulinda jamii nzima. Ndiyo maana tumeleta wataalamu wetu kutoa elimu moja kwa moja hapa Sabasaba,” alisema.
Kwa ujumla, FCC inatumia jukwaa la Sabasaba sio tu kusimamia ushindani wa haki, bali kama daraja la kuunganisha elimu, usalama wa jamii na kukuza mazingira bora ya biashara kwa Watanzania wote.
