Shirika la ulinzi wa raia la Gaza limetangaza kuwa operesheni za kijeshi za Israel zimesababisha vifo vya watu 32 katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa msemaji wa shirika hilo jana, Mahmud Bassal, watu wanane wameuawa kwenye mashambulizi mawili yaliyolenga shule katika mji wa Gaza na wengine wanane waliuawa karibu na kituo cha kugawa misaada kusini mwa Gaza.

Mashambulizi hayo yanajiri saa chache baada ya kundi la Hamas kusema kuwa liko tayari kuanza mazungumzo “mara moja” kuhusu pendekezo la kusitishwa mapigano lililoletwa na Marekani.

Hata hivyo afisa wa Israel baada ya kupokea taarifa ya Hamas amesema hakuna uamuzi wowote kuhusiana na mwitikio wa pendekezo la Hamas la kusitisha mapigano.

Haya yanajiri huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akitarajiwa kusafiri kuelekea Washington kwa mazungumzo siku ya Jumatatu na Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye amezidisha juhudi za kutafuta suluhisho vita vya hivyo vya muda mrefu.