Na Mwandishi Wetu
Wadau wa sekta ya utalii, mazingira na maendeleo ya jamii wameitaka Serikali na mashirika ya kimataifa kuweka msukumo maalumu kuhakikisha mbio za Great Ruaha Marathon zinapandishwa hadhi na kuwa tukio la kimataifa.
Hatua hiyo imeelezwa itasaidia kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kimataifa, kukuza utalii wa ndani na nje, pamoja na kuhamasisha uhifadhi wa maliasili na maendeleo ya jamii zinazozunguka hifadhi hiyo.
Hoja hiyo imetolewa kwenye kilele cha mbio hizo zilizofanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, zikihudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Heri James, pamoja na Kamishna Mkuu wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Musa Kuji.

Akitoa hoja hiyo, Kamishna Musa Kuji alisema kuwa TANAPA inaendelea kuona mafanikio ya mbio hizo kila mwaka, na kwamba ni muda sasa Great Ruaha Marathon ipandishwe daraja na kuwa ‘Great Ruaha International Marathon’ ili kufikia hadhi ya kimataifa na kuvutia washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani.
“Marathon hii ni sehemu ya kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambayo ni miongoni mwa vivutio muhimu vya utalii nchini na barani Afrika. Serikali iko nyuma yetu – Mheshimiwa Waziri Mkuu yupo, Mkuu wa Mkoa na viongozi wote wa mkoa wapo nasi. Hii ni fursa ya kipekee,” alisema Kamishna Kuji.
Alifafanua kuwa Hifadhi ya Ruaha ilikuwa ikichangia chini ya asilimia 10 ya mapato ya TANAPA kwa mwaka, lakini sasa mchango wake unaongezeka kutokana na mikakati madhubuti ya utangazaji ikiwa ni pamoja na mbio hizo.
“Hifadhi hii sasa imeanza kuonyesha mafanikio makubwa. Tuna tuzo saba za kitaifa, mbili kutoka ukanda wa kusini ikiwemo moja ya Ruaha na nyingine ya Kitulo. Haya ni mafanikio ya kushirikisha jamii na kuifanya hifadhi iwe sehemu ya maisha yao,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alieleza kuridhishwa kwake na mbio hizo na kuzitaja kuwa ni tukio kubwa la kitaifa.
Alitoa wito kwa Watanzania kushiriki kwa wingi katika matukio ya namna hiyo ambayo yanachangia kuongeza pato la taifa kupitia utalii na huduma nyingine.
“Mbio hizi ni jukwaa la kutangaza vivutio vyetu, lakini pia ni nafasi ya kuwakutanisha wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla. Zinapaswa kuungwa mkono zaidi ili zifikie hadhi ya kimataifa,” alisema Waziri Mkuu.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Iringa, Peter Jackson alisema ukuaji wa sekta ya utalii umeongeza mapato ya Serikali na kuchochea maendeleo ya miundombinu.
“Uwanja wa ndege sasa umekamilika na barabara ya kuelekea hifadhini imeanza kujengwa. Hii inamaanisha sasa hifadhi hii itafikika kirahisi, na TRA tunatarajia mapato kuongezeka zaidi kutokana na watalii na wawekezaji wanaovutiwa kuja,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la Sustainable Youth Development Program (SYDP), Edward Athanas linaloratibu mbio hizo alisema zinafanyika mara moja kwa mwaka kutokana na changamoto za kifedha, lakini matarajio ni kuwa na matukio mengi zaidi kama ufadhili utaongezeka.
“Kaulimbiu yetu ni ‘Tumerithishwa, nasi tuwarithishe’. Huu ni mwendelezo wa kuwajengea jamii zinazozunguka hifadhi uelewa kuhusu uhifadhi na pia kutumia michezo kama chachu ya maendeleo.”
Aliishukuru Benki ya TCB na wadau wengine kwa udhamini wao mwaka huu, na akaomba apatikane mdhamini mkuu wa kudumu kwa ajili ya kuifanya Great Ruaha Marathon kuwa endelevu na yenye mvuto wa kimataifa.
“Tunaomba pia Benki ya Dunia na UNDP watusaidie kwa kuwa tukio hili linahusisha utunzaji wa mazingira. Tunahitaji pia TTB (Bodi ya Utalii Tanzania) kutuweka kwenye kalenda yao rasmi ya matukio ya utalii,” alisema.

Walezi wa mbio hizo ni Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu na Mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi ambaye pia alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mbio hizo kwa ushirikiano wa ndani na nje ya nchi.
“UNDP ni sehemu ya maendeleo ya nchi. Tunahitaji mashirika haya ya kimataifa yaendelee kuwekeza katika matukio haya ambayo yanaongeza uelewa wa jamii na kuimarisha uhifadhi,” alisema Chumi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje.
Kwa upande wao, UNDP walisema wanaunga mkono jitihada za kulinda wanyamapori kupitia programu ya Wide Ranger ambayo inalenga kudhibiti ujangili na kuimarisha ulinzi wa maeneo ya hifadhi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Heri James alimwambia Waziri Mkuu kuwa yeye ni balozi rasmi wa mbio hizo, na kwamba ofisi yake iko tayari kushirikiana na TANAPA, SYDP na wadau wengine kuhakikisha Ruaha Marathon inazidi kupata nguvu ya kimataifa.
Aliswna mbio za Great Ruaha Marathon zinaendelea kukua kila mwaka, zikiakisi muunganiko wa michezo, uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii — ikiwa ni sehemu ya mageuzi chanya yaliyochochewa pia na programu ya Royal Tour.
“Matarajio ni kwamba, kwa ushirikiano wa wadau wa ndani na nje, mbio hizi zitaingia kwenye kalenda ya matukio makubwa ya kimataifa na kuwa kivutio kikuu cha utalii katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania,” alisema.