Kila mwaka ifikiapo Julai 7, Kenya huadhimisha Saba Saba,kama siku iliyokita mizizi katika mapambano ya muda mrefu ya demokrasia .
Kilichoanza mwaka wa 1990 kama maandamano ya kijasiri dhidi ya utawala wa chama kimoja wa rais wa awamu ya pili Kenya Rais Daniel Arap Moi kimekua na kuwa ishara yenye nguvu ya upinzani, uharakati wa raia, na mapambano yanayoendelea ya haki.
Saba Saba, inawakilisha tarehe 7 Julai, na inatumika kama ukumbusho mkubwa wa kujitolea kwa Wakenya katika mapambano ya demokrasia ya vyama vingi.
Historia ya Saba Saba
- Mwaka 1990, Kenya ilikuwa ikifanya kazi chini ya mfumo wa chama kimoja ulioongozwa na hayati Rais Daniel Arap Moi kupitia cha kimoja cha KANU.
- Upinzani wa kisiasa ulipigwa marufuku, na uhuru wa vyombo vya habari ukawekewa vikwazo vikali. Zaidi ya hayo, kuchanganyikiwa kwa umma kuliongezeka, kutokana na usimamizi mbaya wa kiuchumi na kutengwa kwa jamii fulani.
- Mnamo Julai 7, 1990, viongozi wa upinzani Kenneth Matiba, Charles Rubia, na Jaramogi Oginga Odinga waliitisha mkutano katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi kudai kurejeshwa kwa demokrasia ya vyama vingi.
- Hata hivyo, serikali ilipiga marufuku mkutano huo, na waandamanaji walikaidi marufuku hiyo, ambayo ilisababisha machafuko makubwa katika jiji hilo.
- Wakati wa maandamano hayo, polisi wa kutuliza ghasia waliwatawanya waandamanaji kwa nguvu, na kusababisha kukamatwa, kuwekwa kizuizini bila kesi na vifo miongoni mwa Wakenya wengi. Matukio ya siku hiyo yakawa hatua ya mabadiliko katika mapambano ya Kenya ya mageuzi ya kidemokrasia.
