Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Salum, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwatia moyo watoto wao kuchangamkia masomo ya sekta ya bahari kutokana na uhaba mkubwa wa mabaharia nchini.
Akizungumza leo katika Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayofanyika katika Viwanja vya Julius Nyerere, Salum alisema kuwa licha ya sekta hiyo kuwa na fursa nyingi za ajira, vijana wengi wanapuuza na kukimbilia taaluma nyingine.

“Sekta ya usafiri majini bado ina nafasi kubwa ya ajira, lakini vijana wamekuwa wakijikita zaidi kwenye fani nyingine. Wazazi na walezi wahamasishe watoto wao kusomea ubaharia,” alisema Salum alipokuwa akizungumza kwenye banda la TASAC.
Ameeleza kuwa ushiriki wa TASAC katika maonyesho hayo una lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu ya wakala huo, ikiwemo udhibiti wa usafiri majini na kuendeleza sekta hiyo kwa manufaa ya taifa.
“Ukitembelea banda letu utapata taarifa kuhusu mfuko wa mafunzo ya sekta ya bahari na fursa za masomo, zikiwemo kwa wanawake. Tunalenga kuwafikia watu wote,” alisema Mkurugenzi huyo Mkuu.

Salum alibainisha kuwa TASAC imekuwa ikihusika na usajili wa vyombo vya majini, kuvipa vyeti vya ubora kwa ajili ya kuendesha shughuli zake, lengo kuu likiwa ni kuhakikisha usalama na ubora wa huduma za usafiri majini.
Pia alieleza kuwa Wakala huo kupitia wataalamu wake hufanya ukaguzi wa meli za kimataifa zinazoingia nchini na kufuatilia shughuli zote katika maeneo ya baharini, ikiwemo kutoa taarifa za uokoaji, hali ya hewa, na tahadhari kwa wavuvi.

“Tunajitahidi kuhakikisha bahari inabaki safi na salama. Usalama wa bandari, utoaji wa leseni na usimamizi wa shughuli za ujenzi wa bandari ni sehemu ya majukumu yetu ya kila siku,” alisisitiza Salum.
Kwa ujumla, TASAC imeendelea kuwa miongoni mwa taasisi muhimu katika kuhakikisha usafiri wa majini unakuwa salama, unaodhibitiwa na unaowezesha fursa za kiuchumi kwa Watanzania wengi, hususani vijana.

