Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KILO 37,197.142 za dawa za kulevya zimekamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), katika kipindi cha mwezi Mei hadi Julai mwaka huu.

Hayo yamesemwa leo na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza bayana kuwa ukamataji wa dawa hizo umetokana na ushirikiano mzuri wa vyombo vya dola.

Alisema DCEA imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini na kukamata dawa za kulevya jumla ya kilogramu elfu 37,197.142 ambapo kilogramu elimu 11,031.42 za dawa mpya za kulevya (New Psychoactive Substance) aina ya Mitragyna Speciosa.

“Pia tumekamata bangi kilogramu elfu 24,873.56, mirungi kilogramu 1,274.47, skanka kilogramu 13.42, heroin kilogramu 2.21 na methamphetamine gramu 1.42. Pia, ukamataji huo umehusisha dawa tiba zenye asili ya kuievya aina ya ketamine kilogramu 1.92, Fluni-trazepam (rohypnol) vidonge
1000, lita 6 za kemikali bashirifu aina ya hydrochloric acid na uteketezaji wa ekari 1.045.5 za mashamba ya bangi,” alisema.

Kamishna Jenerali Lyimo alisema kadhalika, kilogram 26 za dawa za kulevya aina ya heroin, zilizokuwa ziingizwe nchini kutokea nchini Msumbiji zilizuiwa.

Alisema watuhumiwa 64 walikamatwa wakihusishwa na dawa hizo.

“Katika operesheni iliyofanyika bandari kavu eneo la Temeke jijini Dar es Salaam, kiliogramu 11,031.42 za dawa za kulevya aina ya Mitragyna speciosa zilizoingizwa nchini kutokea nchini Sri Lanka zilikamatwa zikiwa kwenye vifungashio vyenye chapa inayoonesha kuwa ndani yake kuna mbolea.

Mitragyna speciosa iko katika kundi la dawa mpya za kulevya zinazotokana na mimea inayofahamika kwa jina la “Kratom” mmea huu unakemikali aina ya Mitragynine na 7-Hydroxymitragynine (7-HMG) ambayo inasifa ya vichangamshi (stimulants) na vipumbaza (depresants) vyenye madhara ya kiafya kwa mtumiaji kwani huathiri mfumo wa fahamu na kusababisha uraibu hata kupelekea vifo vya ghafla,” alisema.

Lyimo alisema katika operesheni iliyofanyika eneo la Posta jjini Dar es Salaam, watuhumiwa sita, wakiwemo raia wawili wa China wanaofahamika kwa majina ya Chein Bai na Qixian Xin walikamatwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine gramu 1.42, dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya frunitrazepam (rohypnol) vidonge 1,000 na Ketamine zenye uzito wa Kilogramu 1.92.

Kamishna Jenerali Lyimo alisema Mkoani Dar es Salaam eneo la Sinza walikamatwa watu wawili wamiliki wa kiwanda bubu kinachotengeneza biskuti zinazochanganywa na bangi kisha kuzisambaza katika mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara.

Alisema wakati huohuo mkoani Lindi alikamatwa mfanyabiashara wa madini akisambaza biskuti zilizochanganywa
na bangi.

“Kwa upande wa dawa za kulevya za mashambani, zilikamatwa jumla ya kilogramu 26,191.45 za bangi, mirungi, skanka na kuteketeza ekari 1,045.5 za mashamba ya bangi katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Mara, Kagera, Dodoma, Tabora, Morogoro na Arusha,” alisema.

Alisema mamlaka imebaini kuwa, baadhi ya wahalifu wa dawa za kulevya wameanza tena kutumia maiti za binadamu kubeba dawa za kulevya, maarufu kwa jina la begi.

Aidha, kumekuwa na matukio ya raia wa kigeni kuwatumia watanzania
kusafirisha au kusambaza dawa za kulevya. Mara nyingi, huanzisha mahusiano ya kirafiki na kisha kuwahusisha katika biashara hii haramu kwa kutumia kampuni zao na vyombo vyao vya usafiri hususani bodaboda, bajaji, Tax na wasambazaji wa vifurushi.

Alisema wananchi wanapaswa kuwa makini na kuchukua tahadhari kubwa hasa pale wanapotumwa au kupokea mizigo kutoka kwa watu wasiowafahamu vyema.

“Ni muhimu mjiridhishe na mizigo wanayoisafirisha ili kuepuka
kujikuta wakihusika katika usafirishaji wa dawa za kulevya. DCEA inawaomba watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya kwa kuwafichua watu wanaojihusisha kwa namna yoyote ile na dawa za kulevya ili tatizo la dawa za kulevya litabaki historia hapa nchini,” alisema.

Lyimo alisema hata hivyo, kwa
yoyote atakayejihusisha na uzalishaji, usambazaji na biashara ya dawa za kulevya, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.