Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WASANII nguli wa muziki wa Bongo Fleva, Said Juma ‘Chege Chigunda’ na Hamad Ally ‘Madee’, maarufu kama Samia Kings, wameinogesha Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kwa kuhamasisha Watanzania kuenzi na kununua bidhaa zenye nembo ya Tanzania.

Wasanii hao walipokelewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dkt. Kedmon Mapana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) katika banda la Karume ambalo limejikita kuonesha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na Watanzania wenyewe kwa ubunifu na viwango vya juu vya ubora.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Madee alisema: “Kama bado uko nyumbani na hujafika kwenye banda letu la Made in Tanzania, umepata dhambi! Kuna vitu vingi sana vya asili yetu ambavyo huwezi kuviona popote. Hii ni fursa ya kipekee kujifunza na kujivunia vyetu.”

Aliongeza kwa kusimulia kisa alichokutana nacho nje ya nchi aliponunua bidhaa zenye asili ya Afrika lakini zikiwa na nembo ya mataifa mengine:

“Nilinunua nyanya na vitunguu ambavyo nilijua kabisa vimetoka Tanzania, lakini ziliandikwa vimetokea nchi nyingine. Hii inaumiza. Ndiyo maana huu mpango wa Made in Tanzania ni ukombozi mkubwa kwa watu waishio nje ya nchi na wenye mapenzi na bidhaa za nyumbani,”.

Kwa upande wake, Chege alitoa wito kwa wazazi kuwapeleka watoto wao kutembelea katika Maonesho hayo na kujionea bidhaa zinazotengenezwa Tanzania.

“Nasikitika sijaja na Binti yangu Jada…ningekuja naye tungenunua bidhaa nyingi za Kitanzania. Watoto wana adopt mapema, hivyo huu ni wakati mzuri wa kuwajengea moyo wa kupenda vya kwao. Nawaomba wazazi wenzangu tuwalete watoto wetu, ndiyo kizazi cha kesho,” alisema.

Chege alieleza kuvutiwa na ubunifu wa mavazi, viatu na bidhaa nyingine za viwandani vinavyotengenezwa hapa nchini.

Naye msanii kutoka Afrika Kusini, aliyeshiriki katika maonesho hayo, alisema amevutiwa na ubora wa bidhaa za Tanzania na kuahidi kuwa balozi wa kuzitangaza kwa wenzake nyumbani.

“Nimeona vitu vya hali ya juu, na nimepata uzoefu mzuri. Nitarudi na kuwaeleza watu wetu Afrika Kusini kuwa Tanzania inatengeneza bidhaa bora kabisa,” alisema.

Awali, Dkt. Mapana, aliwahimiza Watanzania kutumia fursa ya Sabasaba kutembelea banda la Karume kujionea ubunifu wa ndani na kushiriki kukuza uchumi wa nchi kupitia bidhaa za ndani.

“Maonesho yanaendelea hadi Julai 13. Muda bado upo, na tunawakaribisha Watanzania wote kutembelea na kujivunia Made in Tanzania,” alisema Dkt. Mapana.

Mbali na kushiriki katika uhamasishaji wa bidhaa za ndani, Chege na Madee pia walitoa burudani ya aina yake kwa mashabiki waliojitokeza katika tamasha hilo la Sabasaba, na kuzidi kuupa umaarufu mpango wa Made in Tanzania unaolenga kukuza viwanda vya ndani, ajira na uchumi wa taifa.