- Kupata Elimu ya Biashara, Viwanda na Kilimo
- Mafunzo yatakayo wafaa baada ya kuhitimu kidato cha Nne
Baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Nne mchepuo wa Biashara kutoka Shule ya Sekondari Mwinyi iliyopo Mkuranga, Mkoani Pwani, wametembelea banda la Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujifunza kuhusu masuala ya biashara, viwanda na kilimo.
Wakiwa katika ziara hiyo ya mafunzo maalumu, wanafunzi hao walipata fursa ya kusikiliza maelezo kutoka kwa Afisa rasilimali watu wa TCCIA, Bi Judith Sarakikya, aliyewaelimisha kuhusu fursa zilizopo katika taasisi hiyo pamoja na namna ya kuanzisha na kuendesha biashara kwa ufanisi.

Bi Sarakikya alieleza kuwa lengo la TCCIA ni kuwaandaa vijana kifikra na kivitendo ili kuwa sehemu ya mabadiliko ya kiuchumi kupitia ubunifu, ujasiriamali na uzalishaji wa bidhaa ndani ya nchi.
“Ni muhimu kuwajengea wanafunzi msingi wa uelewa kuhusu biashara na viwanda mapema, ili waweze kutumia elimu wanayopata shuleni kwa vitendo pindi watakapomaliza masomo yao,” alisema Bi Sarakikya.
Maonesho ya Sabasaba ni jukwaa muhimu la kujifunza, kubadilishana maarifa na kufahamu fursa mbalimbali za kiuchumi, na mwaka huu yamevutia taasisi nyingi za kielimu na wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali nchini.



