Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Mkoa wa Shinyanga umepokea zaidi ya shilingi trilioni 1.563 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo huduma za jamii ,sekta za afya, elimu, miundombinu, maji, kilimo, nishati, madini, mifugo, ardhi na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Hayo yameelezwa leo July 14,2025 Jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mohamed Mhita, wakati akieleza mafanikio ya serikali ya awamu ya Sita kwa kipindi cha miaka minne kwa waandishi wa habari.

Amesema, “Kwa namna ya pekee tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti unaoleta tija kwa wananchi wetu,” amesema Mhita.
Amesema kwa kipindi cha miaka minne Mkoa wa Shinyanga umekusanya mapato ya ndani ya takribani bilioni 150.26, sawa na asilimia 98 ya lengo, huku miradi ya thamani ya bilioni 65.5 ikitekelezwa kupitia mapato hayo.
Aidha, sekta ya madini pekee imechangia mapato ya zaidi ya bilioni 540, huku TRA ikikusanya bilioni 202.54, ikiwa ni zaidi ya lengo kwa asilimia 102.
Kwa upande wa sekta ya afya, ameeleza kuwa serikali imewekeza bilioni 79.1 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya, ambapo hospitali za wilaya zimeongezeka kutoka mbili hadi saba, na vituo vya afya kutoka 25 hadi 38.

Amefafanua kuwa Zahanati pia zimeongezeka kutoka 226 hadi 277, huku upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ukipanda kutoka asilimia 76 hadi 88.
“Elimu nayo imepata kipaumbele kwa kupokea bilioni 155.24 zilizotumika kujenga shule, madarasa, maabara, maktaba na mabweni. Idadi ya shule za msingi imeongezeka hadi 711 na sekondari kufikia 200, huku walimu wapya 1,215 wakiajiriwa, ” ameeleza.
Kwa upande mwingine ameeleza kuwa huduma ya maji imeboreshwa kwa kiasi kikubwa, kufuatia uwekezaji wa bilioni 113.33, ambapo vijiji vyenye huduma ya maji vimeongezeka kutoka 162 hadi 384, huku miradi 64 ikikamilika.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Shinyanga amesema Katika sekta ya kilimo na mifugo, Mkoa umeongeza uzalishaji wa mazao na maziwa, na kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora na zana za kisasa, pamoja na ujenzi wa majosho 16 na mashamba darasa manne ya malisho.

“Mkoa umeimarisha sekta ya madini ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka tani 7.9 hadi 42.5 na fedha za kigeni kutoka Dola milioni 44 hadi 191,Halmashauri zimeongeza mapato kutoka milioni 745 hadi bilioni 3.3, huku vituo vya ununuzi wa madini vikiongezeka kutoka sita hadi 12,”amesema.
Kwa upande wa miundombinu, Mhita amesema barabara za lami zimeongezeka kutoka kilomita 224 hadi 281, changarawe kutoka 957 hadi 1,411, madaraja kutoka 45 hadi 57, na taa za barabarani 611 zimesimikwa. Zaidi ya bilioni 221.19 zilitumika kwenye sekta hii.
Amesema Nishati pia imeimarika kwa kuunganisha vijiji vyote 506 na vitongoji 982 kwa umeme, huku TANESCO ikipokea bilioni 492 kufanikisha hilo.
“Katika ardhi, Mkoa umepima viwanja 10,658 na kutoa hati miliki zaidi ya 20,000, na vijiji 116 vimepata mipango bora ya matumizi ya ardhi.

Kwa upande wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, mikopo yenye thamani ya bilioni 8.56 imetolewa kwa vikundi, huku kaya 35,055 zikinufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini kwa zaidi ya bilioni 59.57,”amesema mkuu huyo wa mkoa wa Shinyanga.
Mbali na hayo ameutaja Miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea kuwa ni pamoja na Mradi wa Umeme wa Jua wa Ngunga (MW 150 – bilioni 323), Upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Ibadakuli (bilioni 52.8), na ujenzi wa barabara ya Kahama-Bulyanhulu-Kakola (km 73 – bilioni 100.6).
“Mkoa wa Shinyanga unasimama kama mfano wa mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020–2025 chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia. Wananchi wetu sasa wanaona matokeo ya uwekezaji katika maisha yao ya kila siku.”amesisitiza

