Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imepokea Tuzo ya shukrani kutoka kwa Taasisi isiyo ya Serikali inayojulikana kama Foundation for Disabilities Hope (FDH) iliyopo Mkoani Dodoma.
Akizungumza katika utoaji wa tuzo hiyo iliyofanyika Julai 14,2025, katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA zilizopo Mkoani Morogoro, Kaimu Kamishna wa TAWA, Mlage Kabange alisema TAWA imekuwa ikishirikiana na FDH katika utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya uhifadhi kwa kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuilinda rasilimali ya wanyamapori na utunzaji wa mazingira katika maeneo ya hifadhi.

Sambamba na hilo, Kamishna Kabange alisema katika kuhakikisha jamii inanufaika na shughuli za uhifadhi, TAWA imeweka utaratibu maalumu wa kuruhusu wananchi kufanya shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki katika baadhi ya maeneo inayosimamia ili kuruhusu wananchi kujipatia kipato kutoka katika uhifadhi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya FDH, Maiko Salali aliishukuru TAWA kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Taasisi yao, Aidha, alisema FDH imekuwa ikitambua mchango wa Taasisi mbalimbali zinazosaidia jamii ya watu wenye ulemavu na TAWA ni miongoni mwa Taasisi kinara ambayo imekuwa ikitoa msaada unaowasaidia makundi hayo kufikia malengo na kutatua changamoto mbalimbali.
Bw. Salali aliongeza kuwa FDH imeguswa na jitihada zinazofanywa na TAWA za kuweka kipaumbele kundi la watu wenye ulemavu hivyo Tuzo hii ni kutambua mchango wa TAWA kwa makundi ya watu wenye ulemavu.
Sambamba na hilo, Bw. Salali alisema FDH itaendelea kushirikiana na TAWA katika kuhamasisha jamii katika utunzaji wa mazingira na kulinda vivutio vya utalii.


