Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Simon Sirro amesema atawapigia wahalifu waliombipu kutokana na kukasirishwa na kitendo cha kuteka magari kilichotokea wilayani Kibondo mwishoni mwa wiki iliyopita na kwamba hatua madhubuti zimechukuliwa kukabiliana na wale wote waliohusika na tukio tukio.
Alisema hayo katika kikao na watumishi wa Manispaa ya Kigoma ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kutembelea wilaya kukagua miradi na kuzungumza na watumishi ambapo alisema kuwa kama wahalifu wamembipu basi yeye anawapigia.
Sirro alisema kuwa taarifa zinaonesha kuwa vitendo vya utekaji vilikuwa vimekomeshwa lakini sasa wahalifu wameonesha kwamba bado wapo hivyo kupitia vikosi vya ulinzi na usalama vitafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha waliofanya uhalifu katika tukio la Kibondo wanakamatwa.
Mkuu wa mkoa Kigoma alisema juzi alikutana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kujadili na kuwekea mkakati tukio hilo sambamba na kuimarisha ulinzi kwenye barabara kuu na ziwa Tanganyika.
Katika mkutano huo na watumishi, mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa kwa sasa hana maneno mengi baada ya tukio hilo lakini majibu yataonekana huku akiwaonya watu wote kutojihusisha na wahalifu na vitendo vya kihalifu kwani sheria kali dhidi yao zitachukuliwa.
Julai 11, mwaka huu watu wanaoaminika kuwa majambazi waliteka basi la abiria la kampuni ya Adventure kilometa mbili kutoka kambi ya wakimbizi wa Burundi ya Nduta, Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma ambapo mali mbalimbali za abiria ziliporwa kwenye tukio hilo.
Baada ya tukio hilo Kamanda wa polisi, Mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu alielekea eneo la tukio na kwamba upelelezi na msako umeanza kuwasaka waliohusika na tukio la utekaji lililotokea Kibondo.
Kamanda Makungu alisema kuwa taarifa walizokusanya kutoka kwa abiria waliokuwa kwenye gari zilizotekwa likiwemo basi la abiria na gari ndogo aina ya Toyota Kluger alisema kuwa majambazi walipora fedha taslimu kiasi cha Sh milioni 3.5, kompyuta mpakato moja na simu tatu za mkononi.
