Na Mwandishi Wetu

Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kuhakikisha watoto wanapata elimu na kusaidia kupunguza idadi ya watoto wa mtaani.

Akizungumza Julai 14, katika shule ya Kibasala jijini Dar es Salaam kwenye ziara iliyohusisha Shirika la GPE (Global Partnership Education) na Taasisi ya Malala Fund inayojihusisha na kuwawezesha wanawake kwenye elimu, Dk Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa GEP amesema katika mafanikio hayo hauwezi kulisahau Shirika la GPE na Malala Fund.

Ameeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa mataifa 91, ambayo GEP inashirikiana nayo na imekuwa kwenye ushirikiano tangu mwaka 2013 na mafanikio yake yanajionesha wazi.

“Tangu tulipoanza ushirikiano na GPE wamefanikisha kujenga madarasa 2,980 vyuo 7,673 nyumba za walimu 64, shule mpya 18, mabweni 15 ya watoto wenye mahitaji maalum, madarasa ya mfano kwaajili ya elimu ya awali 300, vituo vya waalimu 252 pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vitabu milioni 36.1,” amesema Dk Kikwete.

Amesema mwaka 2014 aliona umuhimu wa kuja na sera ya elimu bure kutokana na uwepo wa sababu mbalimbali zinazokwamisha watoto kupata elimu, hivyo licha ya kwamba alikaribia kustaafu alihakikisha sera hiyo inafanya kazi katika awamu iliyofuata na matunda yake yanaonekana sasa kwani tangu mwaka huo idadi ya wanafunzi shuleni pamoja na vyuoni imeongezeka kwa kiasi kikubwa na ufaulu umeongezeka lakini bado wanaendelea kufanya kazi,.

‘‘Tunataka tufike mahali tusiwe na division sifuri hata moja huo ndio mpango wetu na tutaendelea kufanya kazi kwenye hilo,”amesema.

Katika hatua nyingine ametoa maelekezo kwa viongozi wote kuhakikisha hakuna anaekwamisha ndoto ya vijana wa kitanzania kupata elimu na kutimiza ndoto zao, huku akiwataka wanafunzi wenyewe kusimamia ndoto zao bila kukata tamaa.

“Ninajua wengi wenu mnapitia changamoto mbalimbali katika masomo yenu, kuna baadhi ya wazazi wanataka kuwaozesha, wengine wanaawambia msifaulu mtihani ili mkaolewe wapate ng’ombe za mahari lakini ninataka kuwaambia kuweni kama Malala kataeni ili mtimize ndoto zenu”

Kwa upande wake kiongozi wa Malala Fund, Malala Yousafzai amesema anajivunia maendeleo yanayoendelea kuonekana katika sekta ya elimu nchini huku akiahidi kuendeleza ushirikiano ili kusaidia watoto wengi zaidi wa kike kufikia ndoto zao.