Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia Dodoma
Katika uzinduzi rasmi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, uliohudhuriwa na viongozi wa juu wa Serikali, wadau wa maendeleo na wananchi, mfanyabiashara maarufu na mwakilishi wa sekta binafsi, Rostam Azizi, amewasilisha salamu zenye msukumo wa kitaalamu na maono ya muda mrefu kuhusu mustakabali wa maendeleo ya Taifa.
Akiipongeza Serikali kwa hatua ya kuandaa dira hiyo muhimu, Rostam amesema dira ni hatua muhimu katika kupanga mustakabali wa nchi, lakini akasisitiza kuwa mafanikio yake yatategemea uwezo wa utekelezaji kwa vitendo, ubunifu na ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na sekta binafsi.
“Kila hatua ya maendeleo huanzia kwenye kupanga,ni wazi kuwa dira hii inatuonyesha ni wapi tunataka kwenda kama Taifa,hili ni jambo la kujivunia Lakini ni lazima tukubaliane, sisi Watanzania tunatazama zaidi namna mpango huu unavyotekelezwa kwa ufanisi,” ameeleza Rostam Azizi.
Ameeleza kuwa moja ya maeneo ya kipaumbele yanayopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa dira hii ni uwekezaji katika rasilimali watu katika kuwajengea uwezo vijana na kuwakuza katika nyanja za uzalishaji, teknolojia, biashara na uongozi.

“Kupitia mpango huu, tutawalea vijana wengi katika nyanja mbalimbali,hatuna budi kuongeza rasilimali watu ili mipango hii iweze kuleta matokeo, Lakini pia, tunahitaji uongozi unaoelekeza ufanisi na unaojengwa juu ya misingi ya amani na utulivu,” amesema.
Amesema Tanzania haiwezi kufanikisha malengo ya Dira ya 2050 kama haitakuwa na uongozi wenye maono, wenye uwezo wa kusimamia utekelezaji wa mipango, na unaojenga mfumo endelevu wa uwajibikaji.
“Tunapowekeza kwenye mtaji wa rasilimali watu, lazima tuhakikishe pia kuwa tuna uongozi wenye nguvu za kuyabeba matarajio yetu na kuyatekeleza bila hivyo, dira inaweza kubaki kwenye makaratasi tu,” ameongeza.
Rostam pia ametumia fursa hiyo kuelezea changamoto zinazowakumba wafanyabiashara nchini na kutoa wito wa kutungwa kwa sera rafiki zitakazowalinda na kuwawezesha, badala ya kuwabana au kuwavunja moyo.
“Hatutafanikisha haya yote kama tutashindwa kuwajali na kuwatetea wafanyabiashara,Sera zitungwe zinazoweza kuwainua, si kuwaumiza,hili ni jambo la msingi kwa ukuaji wa uchumi wetu,” amefafanua kwa msisitizo.
Licha ya hayo amefafanua kuwa mafanikio ya kiuchumi hayawezi kujengwa juu ya mazingira ya kisasi au ubaguzi wa ki sera, bali kwa kuwezesha kila Mtanzania kushiriki na kunufaika na uchumi wa nchi.
“Tukiweza kuwekeza haya, fedha zitakazopatikana zitaendeleza maendeleo na si visasi,hii ndiyo njia ya kujenga mshikamano wa kitaifa,” amesema Rostam.
Ameihakikishia Serikali kuwa sekta binafsi itaendelea kuwa mshirika wa karibu, si tu katika kushauri, bali pia katika utekelezaji wa dira hiyo, ili kuhakikisha inaakisi maisha ya Watanzania wa sasa na wa vizazi vijavyo.
“Sisi sekta binafsi tunaipongeza Serikali na Tume yake ya Mipango kwa kazi kubwa,tuendelee kujenga taifa lenye misingi imara ya maendeleo,Sina shaka kuwa Mheshimiwa Rais utatuwekea misingi mizuri na imara itakayowawezesha watakaokuja baadaye kuendeleza dira hii kwa vitendo,” amehitimisha kwa matumaini.