Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambayo pia ni Hospitali ya Ubingwa Bobezi nchini, Dkt. Delilah Kimambo amesema mipango na mikakati ya hospitali hiyo imefungamanishwa na matarajio ya Dira ya Taifa ya Tanzania ya mwaka 2050.
Akizungumza mapema leo Julai 18, 1025 Jijini Dar es Salaam wakati akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kuzindua Dira hiyo inayolenga upatikanaji endelevu wa huduma bora za afya na mtindo wa maisha unaozingatia misingi ya afya inayokubalika.

“Katika kutekeleza matarajio ya Dira 2050, tumejipanga kuijenga upya MNH kimfumo na miundombinu ambapo kiasi cha fedha TZS. 1.2 Trilioni zitatumika ili iweze kuwa kitovu cha kikanda katika utoaji huduma bobezi za afya zinazokidhi mahitaji ya ndani na nje ya nchi na kuvutia utalii wa kimatibabu pamoja na matumizi sahihi ya teknolojia za kisasa kama vile akili unde” amesisitiza Dkt. Kimambo.
Aidha DKT. Kimambo amesema kuwa Sekta ya Afya ni kipaumbele namba 4.2.2 cha Nguzo ya Pili ya Dira 2050 ambayo pamoja na mambo mengine inalenga upatikanaji wa huduma bora kwa kuimarisha mifumo ya afya inayotumia teknolojia ili kutoa matokeo mazuri ya huduma zenye ubora, nafuu na zinazopatikana kwa wote.
Ameongeza kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake, Hospitali hiyo imejenga utamaduni wa uwajibikaji, kuzingatia weledi na ubunifu katika utendaji wa kila siku ili kuifikia Tanzania ya 2050.