Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Shinyanga

Makada watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wameandika barua kupinga kujumuishwa kwa jina la mmoja wa watia nia wa kugombea ubunge katika orodha iliyopelekwa Dodoma.

Wakizungumza na JAMHURI Digital, makada hao, Michael Jagadi Masanja, John Katambi Jibusa na Jinamabi Pastory wanamtaja mtia nia, Lucy Mayenga kuwa ndiye aliyedanganya katika kujaza kipengele cha tabia na maadili kwenye fomu ya mgombea au mtia nia wa CCM.

“Tumeandika barua kwa Katibu wa CCM Kishapu kupinga kuwamo kwa jina la Lucy miongoni mwa majina yaliyopelekwa Dodoma kwa ajili ya mchujo kabla ya kura za maoni, kwa sababu amewahi kushitakiwa na kuhukumiwa mahakamani,” anasema mmoja kati ya makada hao.

Barua yao ya Julai 4 mwaka huu (nakala tunayo), inasomeka:

“Tunapenda kukutaarifu kuwa mgombea ubunge Kishapu ana kesi na alishahukumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Februari 2023 katika shauri la madai Namba 20 la mwaka 2021.

“Kimaadili si sahihi kumteua mgombea wa namna hii kwa sababu chama kinaweza kupoteza jimbo.”

JAMHURI limeonyeshwa nakala inayodaiwa kuwa ni ya hukumu dhidi ya Lucy iliyosainiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Athuman Matuma.

Mlalamikaji katika shauri hilo ni Kampuni ya Gat Engineering dhidi ya Lucy Mayenga na Cassian Fidelis.

Akizungumzia sakata hilo, Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Odilia Batimayo, amewataka makada na wanachama wengine kuwa wavumilivu kwa kuwa muda wa kuweka pingamizi kwa wagombea bado upo.

“Vikao vinavyofanyika ni vya siri, sasa wao wamejuaje kama amepitishwa? (JAMHURI) Mnapaswa kujiridhisha kwanza kabla ya kuandika kwa kuwa siku majina yatakapotangazwa na jina la mgombea lisiwemo, itakuwa aibu kwenu,” anasema Odilia bila kuweka wazi iwapo ameipata barua ya malalamiko hayo.


Malalamikiwa, Lucy Mayenga, alitafutwa kwa njia ya simu ya mkononi kutaka kujua ukweli kwa upande wake.

Baada ya kujitambulisha na kuzungumza masuala ya kawaida, mwandishi akataka kujua iwapo katika fomu ya maadili, Lucy alikana kuwahi kuwa na kesi ya madai.

Swali hilo halikupokewa vyema na Lucy ambaye awali alikuwa mchangamfu na mwenye bashasha, kwani alikata simu, na alipopgiwa tena, akajibu kwa kifupi: “Niko barabarani kijijini, nitakutafuta nikifika.”
Hata hivyo, Lucy, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, hakupiga tena simu kama alivyoahidi.

Kipengele kimojawapo cha tabia na maadili kwenye fomu inayojazwa na mgombea au mtia nia wa CCM kinamtaka kueleza iwapo amewahi kupatikana na hatia katika kosa lolote la jinai au madai mbele ya vyombo vya dola vya kutoa haki.