Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MASHINDANO ya gofu ya kumuenzi nyota wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake, marehemu Lina Nkya, yameanza kwa kishindo katika Viwanja vya Lugalo, jijini Dar es Salaam, huku wachezaji 150 kutoka kona mbalimbali za nchi wakishiriki.

Shindano hilo ambalo linafanyika kwa msimu wa nne, limeandaliwa na familia ya Said Nkya kwa lengo la kuenzi mchango wa Lina aliyewahi kuiwezesha Tanzania kutwaa taji la Afrika Mashariki na Kati mwaka 2011. Lina alikuwa sehemu ya kikosi kilichoipeperusha vyema bendera ya taifa katika mashindano yaliyofanyika Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mratibu wa mashindano hayo, Ayne Magombe, jumla ya wachezaji 68 wa kulipwa na chipukizi pamoja na 82 wasindikizaji wamesajiliwa kushiriki. Amesema mashindano yalianza Julai 17 na yanatarajiwa kufikia tamati Julai 20, mwaka huu.

“Mashindano ya Lina Tour ni ya kila mwaka, na kwa sasa tunayo matano kwa mwaka. Tunaamini tukipata sapoti zaidi kutoka kwa wadau, tutapanua wigo na kuongeza mashindano mengi zaidi,” amesema Magombe na kutoa wito kwa mashabiki wa gofu kujitokeza kwa wingi.

Mchezaji kutoka klabu ya Kilimanjaro, Racheal Mushi, amesema amejiandaa vema na ana matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mashindano hayo. Ametoa wito kwa vijana kujitokeza kushiriki mashindano hayo kwa ajili ya kukuza vipaji.

Kwa upande wao, wachezaji wa kulipwa kutoka klabu za Gymkhana na Lugalo wamesema wamejiandaa ipasavyo na wanatarajia ushindani mkali huku kila mmoja akiwa na kiu ya kutwaa ushindi ili kumuenzi vyema marehemu Lina Nkya.