Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Zaidi ya shilingi bilioni 80 zimetumika kutekeleza miradi ya maendeleo ya kijamii katika Mkoa wa Mara katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Uwekezaji huo umejikita katika kuboresha huduma za jamii, miundombinu ya masoko, barabara, vituo vya afya, pamoja na uwezeshaji wa vikundi vya wananchi kiuchumi.

Akizungumza Jijini hapa leo July 18,2025 wakati akieleza mafanikio ya miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, amesema kuwa Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa masoko matano ya kisasa, barabara zenye urefu wa kilomita 1,137 na utoaji wa mikopo isiyokuwa na riba kwa vikundi maalum.
Kanali Mtambi amesema zaidi ya kaya 60,000 kutoka wilaya zote tisa za Mkoa wa Mara zimenufaika na ruzuku kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), huku zaidi ya vikundi 1,300 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vikipewa mikopo ya shilingi bilioni 4.2 kutoka halmashauri zao kwa ajili ya kukuza uchumi wa kaya.
Katika nyanja ya miundombinu, Kanali Mtambi amebainisha kuwa Mkoa umejenga masoko ya kisasa katika wilaya za Serengeti (Mugumu), Tarime (Nyamwaga), Butiama (Kwaya) na Rorya, sambamba na ujenzi wa gati na ghala la kisasa katika Bandari ya Musoma kwa ajili ya kuongeza kasi ya biashara kupitia Ziwa Victoria.

“Mafanikio haya ni matokeo ya uongozi madhubuti wa Rais Samia ambaye amewekeza kwa vitendo katika maeneo ambayo yana athari ya moja kwa moja kwa maisha ya wananchi,” amesisitiza Mtambi.
