Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
JESHI la polisi mkoani Pwani, linawashikilia watuhumiwa 17 wakiwemo waliokuwa viongozi wa Serikali za mtaa kwa kosa la mauaji ya Sebastian Moshi (33) mkazi wa Ubungo, Kibangu jijini Dar es salaam yaliyotokea, kata ya Mapinga, wilayani Bagamoyo ,mkoani Pwani.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Salim Morcase alieleza, tukio hilo limetokea julai 15 mwaka huu, huko maeneo ya Tungutungu, kata ya Mapinga, Bagamoyo Imani Godfrey Mmasi (41) mkazi wa Sinza Dar es salaam alifika kwenye eneo lake lenye ukubwa wa hekari 10 akiwa na walinzi wake ili kufanya usafi na kuweka mipaka.
“Wakiwa wanaendelea na zoezi hilo lilifika kundi la watu wanaodhaniwa kuwa wavamizi wa mashamba idadi ambayo haikufahamika mara moja na kuanza kuwashambulia kwa kupigwa na kuchomwa na kukatwa na vitu vya ncha kali”
Kutokana na tukio hilo, Ismail Abbas Omary (45) alipata majeraha makubwa ambapo anaendelea na matibabu hospital ya Rufaa ya Tumbi.

Morcase alieleza, chanzo cha tukio ni uvamizi holela wa ardhi na ametoa wito kwa Wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
Wakati huohuo katika tukio jingine la mauaji,jeshi hilo linamshikilia Rajabu Musa (23) mkazi wa mtaa wa Muheza,Kibaha kwa mauaji ya baba yake mzazi Hamis Said (50) .
Morcase alifafanua kuwa, mnamo 11,julai 2025 saa sita usiku, mtuhumiwa alimshambulia baba yake mzazi, kwa kumpiga ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kumtumbukiza kwenye shimo la choo.
Morcase alibainisha, chanzo cha mauaji hayo bado kinachunguzwa na mara baada ya upelelezi kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.