MTENDAJI wa Kijiji cha Ulowa Namba Moja, Kata ya Ulowa, Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Juliana Mkumbo (30) anadaiwa kujiua kwa kunywa sumu ya panya.
Kamanda wa Jeshi la Polisi, Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi huku akieleza baada ya Juliana kutoonekana siku moja nyumbani kwake waligonga mlango kwa muda mrefu lakini haukufunguliwa ndipo ukavunjwa.
Kamanda Magomi alisema walipoingia ndani walimkuta amelala huku matapishi yake yakiwa pembeni na jeshi la polisi lilifika na kuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka hospitali ya Kahama kwa ajili ya uchunguzi na majibu yalibainika kuwa amekunywa sumu ya panya.
“Mwili wake umefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama na uchunguzi wa awali umebainisha kuwa mtendaji huyo alifariki baada ya kunywa sumu ya panya. Lakini bado tunaendelea na uchunguzi ili kubaini zaidi chanzo cha kifo chake,” alisema Magomi.
Alisema jeshi hilo limesikitishwa na uamuzi aliouchukua mtendaji huyo kwani umri wake bado ni mdogo na alikuwa anategemewa na taifa katika kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Rashidi Kavululu alisema taarifa ya tukio hilo alizipata kutoka kwa mtendaji wake wa kata baada ya kumpigia simu Juliana kwa muda mrefu bila kupokea simu yake kwa muda wa siku mbili mfululuzo.
Kavululu alisema Julai 14 alimpigia simu Juliana kwa ajili ya kupeana maelekezo ya kazi lakini simu yake ilikuwa kama inatumika siku nzima na siku iliyofuata alipiga tena lakini haikupokelewa na kuchukua hatua ya kumpigia mtendaji ili ampigie na kumueleza kuwa anamtafuta na kupokea ujumbe kuwa amefariki.
Alisema majibu hayo aliyapata usiku wa saa nne Julai 16 na kuelekea nyumbani kwa marehemu na kukuta watu wengi na kila mmoja alikuwa akizungumza lake na Polisi walifika na kuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya taratibu za uchunguzi ili kubaini chanzo.
