Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mkoa wa Geita umepokea kiasi cha Shilingi trilioni 1.44 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambazo zimetumika kwenye sekta mbalimbali kama afya, elimu, miundombinu, kilimo, maji, nishati, utalii, uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na miradi mikubwa ya kimkakati.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela ameeleza hayo leo July 21,2025 Jijini Dodoma ambapo amesema mchango mkubwa umetokana na dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwaletea wananchi maendeleo yanayoonekana.

Kwa upande wa sekta ya Afya amesema
Geita imeshuhudia ongezeko la vituo vya afya kutoka 25 mwaka 2021 hadi 42 mwaka 2025, huku zahanati zikiongezeka kutoka 129 hadi 198.

Amesema Vituo hivyo vinasaidiwa na ujenzi wa hospitali za wilaya katika halmashauri zote na majengo ya kisasa kama ICU, EMD na nyumba za watumishi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umeimarika kutoka asilimia 80 hadi 90.

” Vifo vya wajawazito vimepungua kutoka 57 hadi 55, huku maambukizi ya VVU yakishuka hadi asilimia 4.9,”amesema.

Ameongeza kuwa Shule za sekondari zimeongezeka kutoka 130 hadi 240, vyumba vya madarasa kutoka 7,206 hadi 10,540, huku uandikishaji wa wanafunzi darasa la kwanza ukiongezeka kutoka 107,519 hadi 334,224.

Aidha Walimu wa shule za msingi wamefikia 9,156 na wa sekondari 3,696. Uwekezaji umefanyika pia kwenye mabweni ya wasichana, maabara, na vyuo vya VETA ambavyo vimeongezeka kutoka kimoja hadi vitano.

Kuhusu sekta ya Maji amesema kwa miaka minne, huduma ya maji imeongezeka kutoka asilimia 65 hadi 75 mijini, na kutoka 61 hadi 65 vijijini na kwamba Miradi 81 ya maji vijijini imekamilika, pamoja na miradi mikubwa kama ule wa Katoro–Buseresere uliosanifiwa kuhudumia watu 68,000.

Amesema uchimbaji wa visima umeongezeka kutoka 299 hadi 389.

Amesema uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 1.44 hadi 1.51, na ya biashara kutoka tani 67,736 hadi 72,820.

” Serikali imenunua pikipiki 153, vishikwambi 175 na vipima udongo 5 kwa maafisa ugani. Uzalishaji wa maziwa umeongezeka hadi lita milioni 35.8, huku nyama ikifikia tani 7,710 mwaka 2025,”ameeleza.

Kwa upande wa uchimbaji madini amesema Sekta ya madini imeingiza zaidi ya dola milioni 92 za kigeni mwaka 2025, huku Halmashauri zikinufaika kwa mapato ya Shilingi bilioni 10.5 kutoka bilioni 6 mwaka 2021.

Amefafanua kuwa Leseni za wachimbaji wadogo zimeongezeka kutoka 903 hadi 9,774. Masoko ya madini yameongezeka mara mbili kufikia 20 mwaka 2025.