Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BENKI ya CRDB imetangaza rasmi kuanza kwa msimu wa nne wa semina ya ‘Instaprenyua’ jukwaa maalum linalolenga kuwajengea uwezo wajasiriamali wanaoendesha biashara kupitia mitandao ya kijamii.

Semina hiyo inatarajiwa kufanyika Jumamosi Julai 26, 2025, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 21, 2025 Kaimu Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Muhumuliza Buberwa, amesema kuwa semina hiyo ni sehemu ya jitihada za benki hiyo kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali kwa kuwapatia mafunzo ya matumizi ya teknolojia ya kisasa na kuwafungulia fursa za mitaji na masoko.

“Tangu kuanzishwa kwa Instaprenyua mwaka 2022, zaidi ya wajasiriamali 3,000 wamepata mafunzo ya msingi kuhusu matumizi ya mitandao kama Instagram, Facebook, TikTok, WhatsApp na X (zamani Twitter) katika kukuza biashara zao. Hili limewawezesha kupanua biashara zao hata kuvuka mipaka ya nchi,” amesema Buberwa.

Amesema kwa mwaka huu, semina hiyo imeboreshwa zaidi kwa kuendana na mabadiliko ya soko na mazingira ya biashara ya mtandaoni.

“Washiriki watajifunza kutoka kwa wakufunzi bingwa katika nyanja mbalimbali za biashara, pamoja na kupata elimu kuhusu usalama wa biashara mtandaoni, huduma za kisasa za malipo, na fursa za mitaji kwa biashara bunifu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki ya CRDB, Joseline Kamuhanda, amesema kuwa semina ya mwaka huu pia itatoa fursa kwa washiriki kusikia hadithi za mafanikio kutoka kwa waliopitia mafunzo hayo katika misimu iliyopita na sasa wamepiga hatua kubwa katika biashara za mtandaoni.

“Hadithi hizi halisi za mafanikio ni motisha kwa wajasiriamali wapya na ni uthibitisho kuwa Instaprenyua si tu semina, bali ni chombo cha kubadilisha maisha na biashara,” ameeleza Joseline.

Benki ya CRDB imesisitiza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha kila Mtanzania anayejishughulisha na biashara za mtandaoni anapata nafasi ya kujifunza, kuunganishwa na fursa, na hatimaye kukuza biashara yake kwa ufanisi zaidi.

Usajili wa kushiriki katika semina hiyo unapatikana kupitia tovuti ya Benki ya CRDB na kwenye kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.