Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji alikutana na Wezi Moyo, Balozi wa Jamhuri ya Malawi nchini Msumbiji kwa lengo la kujitambulisha na kuzungumza masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi.

Balozi Moyo alimkaribisha Balozi Hamad Jijini Maputo na kumhakikishia ushirikiano kwa muda wote akitekeleza majukumu yake na kuahidi kuendeleza ushirikiano (bilateral relations) wa kidugu na kihistoria baina Tanzania na Malawi.

Aidha, Mhe. Balozi Moyo kwa niaba ya nchi yake aliishukuru Serikali na Wananchi wa Tanzania kwa ushirikiano na misaada mbalimbali ya kijamii inayotoa kila inapotokea mahitaji, akitoa mfano Eneo Maalum la Mizigo ya Malawi (Malawi Cargo) kwenye Bandari ya Dar es Salaam, walilopewa tokea wakati wa Utawala wa Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere.

Mwisho, alisisitiza haja ya kuendelezwa na kuimarishwa miradi mbalimbali ya ushirikiano na kimkakati ikiwemo ya miradi ya miundombinu na nishati, kati ya Tanzania na Malawi kwa maslahi ya Serikali na wananchi wa nchi hizi mbili.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Hamad alimshukuru Mhe. Balozi Moyo kwa kukubali kukutana naye na makaribisho mazuri aliyopewa. Aliahidi kufanya naye kazi kwa ukaribu ili kufanikisha malengo ya nchi zao. Aidha, alieleza nia ya Serikali ya Tanzania kupitia Ubalozi wake Maputo kuendeleza uhusiano mzuri na wa kidugu pamoja na miradi ya pamoja ya kimkakati.

Kuhusu uhusiano wa Kikanda, Mhe. Balozi Hamad alisisitiza juu ya ushirikiano hususan masuala yaliyopo chini ya Mwamvuli wa Jumuiya ya SADC na kushauri Nchi Wanachama (ikiwemo Malawi) kushirikiana katika mapambano dhidi ya ugaidi Kaskazini mwa Msumbiji na maeneo mengine ya jirani. Alitoa rai kwamba kwa kuwa Ugaidi hauna mipaka, ni vyema nchi hizo zikashirikiana katika kukabiliana nao, ikiwemo kubadilisha taarifa (kuhusu ugaidi) na kudhibiti mipaka.