Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum kwa njia ya mtandao kesho, Julai 26, 2025, kwa lengo la kujadili ajenda moja kuu ya marekebisho madogo ya Katiba ya Chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 25,2025 jijini Dodoma , Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, amesema mkutano huo umetangazwa kwa mujibu wa Ibara ya 99 (1)(a-f) na (2) ya Katiba ya CCM, ambayo inaruhusu kufanyika kwa mkutano maalum wa namna hiyo wakati panapotokea haja ya kufanya marekebisho ya Katiba.

Amesema, “Wanaoruhusiwa kufanya marekebisho ya Katiba ya CCM ni Mkutano Mkuu pekee,Kwa kuwa uongozi umeona kuna umuhimu wa kufanya marekebisho haya madogo, tumewaita wajumbe kwa njia ya mtandao ili kujadili na kupitisha mabadiliko hayo,” amesema Makalla.
Ameeleza kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika na kuwa mkutano huo utaendeshwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ambayo itahakikisha ushiriki wa wajumbe wote bila changamoto zozote za kiufundi.
Aidha, Makalla amesema kuwa CCM ni chama kinachoendana na mabadiliko ya dunia ya sasa, hivyo kutumia njia ya kidigitali katika maamuzi makubwa kama haya ni sehemu ya kuakisi mageuzi ndani ya chama.
“Kumekuwa na maswali mitandaoni kuhusu kwa nini mkutano unafanyika mtandaoni. Ukweli ni kwamba dunia imebadilika na sisi hatuwezi kubaki nyuma. Tunawahakikishia kuwa kila kitu kiko tayari na mkutano utaendeshwa kwa mafanikio,” ameeleza.
Hata hivyo, hakutaja kwa kina ni vipengele gani vya Katiba vitafanyiwa marekebisho, lakini alieleza kuwa mabadiliko hayo ni madogo na yataletwa mbele ya wajumbe kwa ajili ya kupitishwa rasmi.
Hatua hiyo ya CCM kutumia mfumo wa mtandao katika kufanya maamuzi makubwa inatajwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha uendeshaji wa shughuli za kisiasa kwa kutumia teknolojia, sambamba na juhudi za vyama vingine vinavyojipanga kisasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.