Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Katika kuhakikisha jamii inapata taarifa zilizo sahihi na zenye usawa kuhusu mwenendo wa haki nchini, Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), imeendesha mafunzo ya kitaalamu kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wa kuripoti habari za kimahakama kwa weledi.

Mafunzo hayo, yamefanyika kwa njia ya mtandao Julai 25, 2025,kwa kuhusisha zaidi ya waandishi 200 nchini ambayo yanatajwa kuwa ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa Mahakama kuhakikisha waandishi wanakuwa sehemu ya mfumo wa haki, kwa kutoa taarifa sahihi, zenye mizania na zisizopotosha.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, amesema waandishi wana mchango mkubwa katika kujenga au kubomoa taswira ya Mahakama mbele ya umma.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo amesema, “Habari moja yenye makosa ya alama au tafsiri potofu inaweza kuharibu heshima ya mhusika au kuzua taharuki isiyo ya lazima,” amesema

Katika mafunzo hayo, Wakili wa Mahakama Kuu na mwandishi mkongwe, Alloyce Komba, amefafanua kwa kina umuhimu wa uelewa wa muundo wa Mahakama kwa waandishi.

Ametoa mfano wa kosa la kawaida ambapo baadhi huandika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, badala ya jina sahihi Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, na kueleza kuwa usahihi huu ni sehemu ya uadilifu wa kazi ya uandishi.

Aidha, amewahimiza waandishi kutambua vyanzo halali vya taarifa za Mahakama, ambavyo ni pamoja na Majaji, Mahakimu, Makarani wa Mahakama, Waendesha Mashtaka, Mawakili na washtakiwa wenyewe.

Pia amekumbusha kuwa kazi ya mwandishi si kutoa hukumu au maoni, bali kuandika kile kilichotokea mahakamani kwa usahihi.

Kwa upande wake, Afisa Habari Mwandamizi wa Mahakama, Faustine Kapama, amesisitiza maadili ya uandishi wa habari za Mahakama, akitaja mambo yanayopaswa kuepukwa kama kuandika majina ya watoto, waathirika na mashahidi kwenye kesi za kingono au udhalilishaji.

Kwa ujumla, mafunzo hayo yamefungua ukurasa mpya katika uhusiano kati ya Mahakama na wanahabari, huku waandishi wakipewa jukumu la kuwa daraja la haki kwa kutumia kalamu zao kuelimisha, kuhabarisha na kulinda utu wa kila mmoja mbele ya sheria.