Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka waandaji wa maudhui mtandaoni kusoma nyaraka mbalimbali na kufuata maelekezo ili ushiriki wao katika mchakato wa uchaguzi uweze kufanyika kwa kuzingatia masharti na matakwa ya sheria .

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji mstaafu wa mahakama ya Rufani  Jacob Mwambegele, alipokuwa akifungua mkutano wa Tume na Wazalishaji maudhui mtandaoni uliofanyika Jijini Dar es Salaam leo Agosti 3, 2025 .

Mwambegele amesema kama waandishi wa mtandaoni katika kipindi hiki cha Uchaguzi ni vyema wakatumia majukwaa yao kuwahimiza wananchi kuwa makini na hawawi chanzo cha kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu.

Amesema  ni ukweli usiopingika kwamba mitandao hasa ya kijamii imekuwa ni chanzo muhimu cha habari na elimu ,hivyo nawaomba kuhakikisha kwamba taarifa mnazoziweka katika kurasa zenu ziwe ni za ukweli na zisizo na chembe ya upotoshaji kwa kuwa ukosefu wa umakini kwenye eneo hili unaweza kuharibu na kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu wakati huu wa uchaguzi .

Pia amesema ni vyema kuepuka matumizi mabaya ya akiliunde ambavyo inatumiwa na baadhi ya watu wenye nia ovu kusambaza habari za upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii.


Tume ina matumaini makubwa ya kufanikisha Uchaguzi huu kwa kutegemea  ushiriki wenu ,imani hii inatokana na ushirikiano mlioonyesha kipindi cha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mmekuwa wepesi wa kuwasilisha hoja na ushauri” amesema.

Amesema INEC itaendelea kuwashirikisha mwa kadri itakavyowezekana ,lengo ni kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 unakuwa huru ,uwazi na haki ili kuamika kwa kuweka mazingira sawa ya ushindani kwaWagombea wa vyama vyote vya siasa vitakavyoshiriki.

Mwambegele amesema Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na.2 ya mwaka 2024 ,Tume inao wajibu wa kutoa elimu ya mpiga kura nchini ,kuratibu na kusimamia Taasisi na Asasi zinazotoa elimu ya moiga kura na kualika na kusajili waangalizi wa Uchaguzi.

“Katika kutekeleza jukumu hilo ,Tume imejipanga kutoa elimu hiyo Kwa njia mbalimbali ambazo ni pamoja na Vyombo vya habari,mitandao ya kijamii, machapisho, mikutano,matamasha kusambaza elimu kwenye halmashauri zote.

Amesema mpaka sasa Tume imeshatoa kibali kwa Taasisi na Asasi 164  za kutoa elimu ya mpiga kura vile vile jumla ya Taasisi na Asasi 76 za ndani na 12 za kimataifa wamepewa vibali vya uangalizi wa uchaguzi.


“Napenda kuwajulisha kuwa majimbo yatakayo tumika kwenye uchaguzi ni 272 ,ambapo majimbo 222 yapo Tanzania Bara na 50 yapo Tanzania Visiwani kwenye idadi hiyo kuna ongezeko la majimbo nane yaliyoanzishwa Tanzania Bara” amesema.

Aidha jumla ya kata 3960 zitafanya Uchaguzi wa Madiwani,kwenye idadi hii kuna ongezeko la kata nne.


Amesema kwa mujibu wa ratiba utoaji wa fomu utaanza tarehe 9 Agosti ,2025 hadi 27 Agosti kwa wagombea wa kiti cha Rais na makamu wa Rais na kuanzia tarehe 14 Augusti ,2025 hadi tarehe 27 Agosti ni utoaji wa fomu za wagombea wa Ubunge na Udiwani na uteuzi itafanyika tarehe 27 Agosti 2025.

Kwa mujibu wa ratiba ya Uchaguzi ,kipindi cha kampeni za uchaguzi kitaanza  tarehe 28 Agosti 2025 hadi 28 Oktoba kwaTanzania Bara na tarehe 27 kwa upande wa Tanzania Zanzibar” amesema.


Mkurugenzi wa Uchaguzi ,Ramadhani Kailiwa amesema waandishi wanayo dhima ya kutoa habari sahihi za ukweli  wakati wa  mchakato wa uchaguzi hivyo wanaombwa kuhakikisha kunakuwepo na taarifa za mara kwa mara za kuelezea kinacho endelea kuhusu uchaguzi.

Kailima amesema kama waandishi wanaweza, kutumia kauli mbinu ya uchaguzi mkuu 2025 kura yako haki yako jitokeze kupiga kura kwenye taarifa zenu itakuwa kama chachu ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi.

*Sisi kama Tume tunawategemea nyinyi waandishi kutoandika, habari zinazoweza kusababisha watu wasione umuhimu wa kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kama wagombea au wapiga kura.