Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), Jaji Mstaafu Jacobs Mwambegele, amewasihi wazalishaji wa maudhui mtandaoni kutumia majukwaa yao kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kampeni na upigaji kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akifungua Mkutano wa siku moja wa Kitaifa kati ya INEC na wazalishaji wa maudhui mtandaoni uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, Jaji Mstaafu Mwambegele alisema lengo la mkutano huo ni kuwajengea uwezo wauelewa wa kutosha wazalishaji hao ili waweze kusambaza taarifa sahihi kuhusu masuala ya uchaguzi.
“Wazalishaji wa maudhui mtandaoni ni wadau muhimu,taarifa wanazochapisha huenea kwa kasi na kuwafikia wananchi wengi. Ni muhimu wakahakikisha habari wanazotoa zinajikita katika ukweli, zinahamasisha amani na zinawaelimisha Watanzania kuhusu haki na wajibu wao katika uchaguzi,” alisema Mwambegele.
Ameongeza kuwa mitandao ya kijamii imekuwa chanzo kikuu cha habari kwa jamii ya sasa, hivyo ni muhimu wazalishaji wa maudhui kutumia fursa hiyo kwa ufanisi, bila kupotosha umma au kusababisha taharuki.

“Mitandao ya kijamii ina nguvu kubwa ya kuathiri maamuzi ya watu,tunawasihi muwe sehemu ya kuhimiza amani, mshikamano na ushiriki wa wananchi kwa njia ya kuwapa taarifa sahihi na zenye maadili,” alisisitiza.
INEC imeahidi kuendelea kushirikiana na wazalishaji wa maudhui na vyombo vingine vya habari ili kuhakikisha taarifa zote zinazohusiana na uchaguzi zinatolewa kwa uwazi, uaminifu na kwa kuzingatia misingi ya sheria na maadili ya uandishi.
Mkutano huo umeandaliwa na INEC kama sehemu ya mkakati wa kuhakikisha mchakato wa uchaguzi mkuu unakuwa shirikishi, wa haki na wa amani, kwa kuwajumuisha wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, wanaharakati wa kidijitali, na wanahabari wa mitandao ya kijamii.
Akitoa mada kuhusu maandalizi ya Uchaguzi huo,Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima amewaasa vyombo vya habari vikiwemo vya waandaaji wa maudhui mtandaoni kutumia nafasi na fursa walizonazo kuhakikisha kunakuwepo na taarifa mara kwa mara za kuelezea kinachoendelea kuhusu Uchaguzi.
Vile vile amewaasa kuzingatiwa Sheria na maadili ya kazi yao katika kutoa taarifa zinazohusiana na masuala ya Uchaguzi lakini pia kutumia kalamu zao kama nyenzo ya kuhubiri amani katika kipindi chote cha Uchaguzi .
