Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama na sahihi ya ndege nyuki (drones) katika shughuli za kilimo, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wake katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

Akizungumza katika banda la TCAA, Mkaguzi wa Ndege Nyuki, Ibrahim Abdalah amesema matumizi ya teknolojia hiyo yameleta mapinduzi makubwa katika kilimo cha kisasa, ikiwemo upuliziaji wa dawa mashambani, ufuatiliaji wa afya ya mazao, uchambuzi wa udongo na utunzaji wa kumbukumbu za mavuno kwa usahihi mkubwa.

“Matumizi ya ndege nyuki katika kilimo yameleta tija kubwa, lakini ni muhimu yaendane na kanuni za usalama na usajili. TCAA tunahakikisha matumizi haya yanafanyika kwa ufanisi bila kuhatarisha usalama wa anga,” amesema Abdalah.

TCAA imesisitiza kuwa kila ndege nyuki inayotumika nchini inapaswa kusajiliwa rasmi na kupata kibali cha matumizi kwa mujibu wa Sheria ya Usafiri wa Anga na miongozo ya matumizi ya ndege hizo.

Aidha, mamlaka hiyo imetoa wito kwa wakulima, watafiti, na watoa huduma wa sekta ya kilimo kutambua fursa iliyopo katika matumizi ya teknolojia hiyo, huku wakifuata taratibu na sheria zilizopo.

“Tunawahimiza wakulima na wadau wote wa kilimo kuwasiliana nasi kwa ushauri, msaada wa kiufundi na kuelewa namna bora ya kupata vibali vya matumizi halali ya drones,” amesema.

Kwa sasa, teknolojia ya drones inazidi kushika kasi katika matumizi mbalimbali duniani, na Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazochukua hatua kuhakikisha matumizi hayo yanakuwa salama, yenye tija na yanayochochea maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi kwa ujumla.