Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki EACOP Umetoa mchango wa shilingi milioni 100 kwa ajili ya matibu ya watoto 25 wenye matatizo mbalimbali ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ikiwa ni sehemu ya kusaidia jamii.
Makabidhiano hayo yamefanyika jana jijini Dar es Salaam katika taasisi hiyo ya JKCI ambapo kaimu Meneja Mkuu wa EACOP Tanzania, Bw. Geofrey Mponda amesema kuwa mojawapo ya sera ya kampuni yao ni kusaidia jamii zenye uhitaji hasa zile zilizopitiwa na mradi.

“Tuliguswa sana na ombi la JKCI la kusaidia watoto wenye uhitaji wa matibabu ya moyo ambapo familia zao haziwezi kugharamia matibabu hayo, hivyo uongozi wa EACOP ukaona kuna kila sababu za kusaidia” alisema Bw Mponda.
Mponda aliongeza kuwa taarifa ya uhitaji katika taasisi hiyo ilikuwa ni watoto 1,500 lakini wamefanikiwa kuanza na hao watoto 25 waliopitiwa na mradi wa bomba la mafuta ghafi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt Peter Kisenge alisema kuwa msaasa huo uliotolewa na EACOP utaenda kurudisha tabasamu kwa familia zaidi ya mia moja kwani kila mtoto anaguswa na familia zaidi ya nne.
“Nipende kuwashukuru sana EACOP kwa huu msaada wao kwetu kwani imekuwa ni ndani ya muda mfupi tangu tutume ombi letu wakalipokea na kulifanyia kazi”, alibainisha Dkt Kisenge.

Dkt kisenge alisisitiza kuwa mahitaji bado ni makubwa kwa watoto wenye changamoto hiyo hiyo, hivyo aliwataka wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa pamoja na taasisi mbalimbali kuweza kutoa msaada kwa watoto hao.
“Tulizunguka katika mikoa 23 kwa ajili ya uchunguzi wa moyo na tulibaini watu wengi sana wana magonjwa ya Moyo, wapo ambao walikuwa wanajua na wengine walikuwa hawajui kama wanachangamoto hizo hivyo ni muhimu kupima afya ya moyo mara kwa mara”, alisisitiza Dkt Kisenge kwa kuonesha ukubwa wa tatizo hilo nchini.
Naye Meneja anayeshughulikia masuala ya Jamii,Mazingira na Uwekezaji wa EACOP Tanzana, Bi. Clare Haule amesema kuwa licha ya kutoa msaada huo pia sera yao ya kusaidia jamii pia imejikita katika kutoa misaada ya kuwawezesha vijana, msaada wa utunzaji wa mazingira pamoja na msaada wa kutoa nishati endelevu.

“Msaada huu wa leo una maana kubwa sana kwani tunaenda kutimiza ndoto za watoto wengi ambao watalisaidia taifa katika Nyanja mbalimbali”, alisema Bi Haule.
Pamoja na hayo, Bw Geofrey Mponda mradi huo umefikia 65% na mpaka kufikia Julai 2026 mradi huo utakuwa umekamilika na kuanza kusafirisjha mafuta ghafi kutoka nchini Uganda mpaka kufika katika Pwani ya Tanga nchini Tanzania.
Washirika wa bomba la mafuta la EACOP ni Total energies likiwa na asilimia 62, Shirika la Maendeleo la Mafuta nchini (TPDC) na Kampuni ya Mafuta ya nchini Uganda (UNOC) kila mmoja akiwa na asilimia 15 pamoja na Kampuni ya kitaifa ya Mafuta ya China (CNOOC) likiwa na asilimia 8.
