Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, wametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kilichotokea leo jijini Dodoma.
Rais Samia kupitia ujumbe aliouandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha kiongozi huyo mkongwe, ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ninatoa pole kwa familia, wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi, watumishi wa Bunge na Wabunge wote aliotumikia nao akiwa Spika wa Bunge letu, wananchi wa Kongwa, ndugu jamaa na marafiki,” ameandika Rais Samia.
Ameongeza kuwa ni wakati wa Watanzania kuungana kumuombea Ndugai, na kuiombea familia yake kuwa na faraja na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu.
“Tuungane pamoja kumuombea kwa Mwenyezi Mungu na kuwaombea familia, ndugu, jamaa na marafiki uvumilivu, faraja na moyo wa ibada katika kipindi hiki kigumu. Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” ameandika Rais Samia.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kupitia taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Raqey Mohamed, amesema amepokea kwa huzuni kubwa taarifa za msiba huo.
“Amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa, Mhe. Job Yustino Ndugai, kilichotokea tarehe 06 Agosti 2025, Dodoma.” imeeleza taarifa hiyo.
Dk. Mwinyi amesema atamkumbuka marehemu Ndugai kwa mchango wake mkubwa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi alizowahi kushika wakati wa uhai wake, hasa katika kulitumikia Taifa kwa moyo wa uzalendo na uadilifu.
Aidha, Dk. Mwinyi ametuma salamu za pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson, familia ya marehemu, wananchi wa Jimbo la Kongwa, pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huo.
“Rais Dk. Mwinyi amewasihi wote waliopatwa na msiba huo kuwa na subira na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” imeeleza taarifa hiyo.
