Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umesema idadi ya kampuni zinazoshiriki kwenye mchakato wa uagizaji wa mafuta zimeongezeka kutoka kampuni 33 mwaka 2021 hadi kampuni 73 mwaka 2025 sawa na ongezeko la asilimia 121.
Mkurugenzi wa wakala huo, Erasto Saimon ametoa takwimu hizo leo Agosti 8, alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ambapo amesema jumla ya zabuni 24 zimesajiliwa katika mfumo wa BPS kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2025.

Erasto amesema kiwango cha uagizaji wa mafuta nchini kupitia mfumo wa BPS kimeongezeka kutoka wastanj wa tani 5,805,193 mwaka 2021 hadi tan6,365,986 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 9.6 hadi disemba mwaka huu jumla ya tani 7,090,165 zitakuwa zimeagizwa sawa na ongezeko la asilimia 11.4
Aidha, Erasto amesema wameshirikikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania ( TPA) kuendelea kupanga ratiba ya meli nchini lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa matumizi ya bandari na kupunguza gharama za meli kusubiri hivyo hatua hiyo imeokoa kiasi dola za marekani milioni 11.5.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deudatus Balile amesema kikao hicho kina manufaa makubwa kwao hivyo kinawapa uelewa zaidi wahariri kuweza kuwajuza wananchi habari kwa kina zaidi.
Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) ni taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Nishati na ilianzishwa kwa mujibu wa sheria ya wakala wa serikali sura 245.











