Na Mwandishi Wetu, Jamhuri Media, Pemba
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah na mgombea Uwakilishi Jimbo la Kiwani amesema kipindi hiki wananchi wanapaswa kuendelea kudumisha amani ili wampe nafasi mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho, Samia Suluhu Hassan aweze kutekeleza majukumu aliyojipangia.
Abdullah ametoa kauli hiyo Septemba 20,2025 alipopewa nafasi ya kuzungumza na maelfu ya wananchi wa Pemba kwenye uwanja wa Gombani ya Kale wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.

Nimepata nafasi ya kuzunguka kule Bara kila nilipokuwa nakwenda jamaa zetu wa kipemba wananifuata, nilikwenda Mtwara wamekuja Wapemba wanazungumza kimakonde, pale Singida na Tabora wanazungumzia kinyamwezi.
Nilifika pale Geita nimeambiwa na mkuu wa mkoa kuna jamaa zako wanataka kukuoma kumbe Wapemba, raha yake sisi tuko kila sehemu duniani, huna sehemu unayokwenda usimkute Mpemba, hii ni kwa sababu ya kazi nzuri inayofanywa na viongozi wetu wakuu hawa.
Niwaombe sana ndugu zangu Wapemba tuache kulishwa sumu na tuache kutiwa maneno ya chokochoko, kugombana na kuchukiana kugombana, sisi sote ni ndugu na sisi ni vijana wa Dk Samia Suluhu na baba yetu Dk Hussein Mwinyi anatupenda sana, yale maendeleo yote ambayo yamesema hapa, yote yanafanywa kwa ajili yetu,amesema.

Amesema kama Bara miradi inavyoendelea ndivyo hivyo hivyo miradi hiyo inaendelea Pemba mchana na usiku, vijijini kuna makampuni ya wakandarasi wanafanya kazi, hakuna sehemu yoyote ambako kazi imesimama.
Naelewa Rais kupata pesa ni jambo, matumizi ya fedha ni jambo jingine, mmekuwa wasimamizi wazuri wewe na Dk. Mwinyi katika matumizi ya fedha za serikali. Si kila anayepata fedha hizi anazitumia vizri wapo wanaopata wanafanya vitu vingi vya ajabu. Ndani ya Jamhuri umetenda haki umetembea mikoa yote nchi nzima umewatendea haki, kila sehemu umeweka kitu,amesema.
