Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo) kimekabidhi kamati ya ushindi magari saba aina ya Toyota Alphard kwa ajili ya kufuatilia matukio yote ya uchaguzi katika wilaya saba za Unguja.
Makabidhiano hayo yamefanywa na Mgombea Urais wa Zanzibar wa chama hicho, Othman Masoud Othman, mjini Unguja wiki iliyopita wakati akizindua timu ya ushindi ya chama hicho kwa kampeni ya ngazi ya urais.
Pamoja na kukabidhi magari hayo, amesema wapo tayari kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu na timu ya ushindi ya chama hicho itafanya kazi katika ngazi zote zikiwamo za wilaya na mikoa.
“Hata kama uchaguzi utaitishwa leo, sisi tupo tayari na tutaibuka na ushindi kwa sababu tupo vizuri katika kuyafikia makundi yote,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji, amesema chama hicho kimejipanga kuleta mageuzi na wapo tayari kwa ajili ya kushika dola kwa kuwa wamejipanga kuleta mageuzi makubwa yatakayowahusisha wananchi moja kwa moja kiuchumi na maendeleo.
Naye Meneja wa kampeni za chama hicho, Ismail Jussa Ladhu, amesema chama hicho kimejifunza mengi katika kipindi cha miaka mitano iyopita ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Sisi tumejipanga tayari kwa ajili ya kuleta mageuzi makubwa ya wananchi ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii, baada ya kuziona kasoro zilizofanywa na CCM katika utawala wa miaka mitano,” amesema.
