CHAMA cha ACT Wazalendo kimesogeza mbele hadi Juni 30, 2025 zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu za nafasi mbalimbali za Uchaguzi Mkuu Tanzania Bara.

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Naibu Katibu Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Shangwe Ayo imeeleza hatua hiyo inalenga kutoa fursa pana kwa wanachama kugombea pia kutoa nafasi kwa wanaokusudia kulitumia jukwaa la chama hicho kulinda na kutetea demokrasia.

“Zoezi la kuchukua na kurejesha fomu kwa nafasi za Zanzibar ambazo ni Urais wa Zanzibar, ubunge kwa upande wa Zanzibar, uwakilishi na udiwani kwa upande wa Zanzibar halitaongezewa muda baada ya kufungwa rasmi tarehe 31 Mei, 2025,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imefafanua kuwa chama kitatoa taarifa ya kina idadi ya wagombea wa nafasi zote waliojitokeza baada ya zoezi la kuchukua na kurejesha fomu upande wa Bara kufungwa rasmi Juni 30, 2025.