Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo ,Othman Masoud Othamn amezindua rasmi Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwa mwaka 2025 -2030 huku akihaidi kurejesha imani kwa Wazanzibar kwa kuweka mbele masuala ya msingi yanayogusa maisha ya kila mwananchi.

Miongoni mwa masuala hayo ni pamoja na elimu bora, huduma bora za afya, ajira zenye tija na staha, hifadhi ya jamii, na uchumi unaowajumuisha wote na kwa jumla na mustakbala mwema wa Zanzibar.

Huku akitaja sera nne za misingi zitakazoinusuru Zanzibar ikiwemo suala la kuchochea uchumi kupitia kilimo na uvuvi wa kisasa, suala la mamlaka na kuifanya Zanzibar kuwa mamlaka kamili, kuimarisha mapambano dhidi ya ufisadi na rushwa na kurejesha utawala wa sheria na thamani ya fedha za umma pamoja na kurejesha utengemano wa kijamii kupitia maridhiano ya kweli na kuongoza mageuzi katika maadili na malezi ya watoto kinyume na silka ya Wazanzibari.

Aliyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari, wahariri pamoja na viongozi wa Chama hicho visiwani Zanzibar wakati wa uzinduzi wa Ilani hiyo.Othman alisema Ilani hiyo iliyozinduliwa ni zao la fikra za pamoja, utafiti wa kitaalamu, na vilio vya wengi, iliyozaliwa kutokana na ari ya kizazi kipya cha wazalendo wanaotaka kuona mwelekeo mpya wa utawala na maendeleo ya Zanzibar.

Amesema kwa miaka mingi, Zanzibar imekabiliwa na changamoto zinazojirudia na zinazohatarisha maisha ya watu wake ikiwemo suala la ukosefu wa ajira kwa vijana,huduma duni za afya na mfumo wa elimu unaoporomoka,utawala wa kibabe usiozingatia maslahi ya wengi,kukosekana kwa utii wa sheria na kufeli kwa mfumo mzima wa kutoa haki.

Tunahitaji mageuzi makubwa ili kurejesha thamani ya utu na maisha ya kila mtu anayeishi Zanzibar kwani dhana ya haki za binadamu na utawala bora imebaki nadharia tu, ikitumika vibaya.

“Kwa miaka mingi Zanzibar imekabiliwa na changamoto zinazojirudia na zinazohatarisha maisha ya watu wake kutokana na uongozi uliopo kushindwa kutoa mwelekeo wa kweli badala yake kutoa ahadi hewa,”amesema Othman.

Aidha, amesema ilani yao imejielekeza katika kuitekeleza dhamira iliyo ndani ya mioyo ya Wazanzibari katika mambo matano ya kipaumbele zaidi ni pamoja na kufanya Mapitio ya Mkataba wa Muungano na Mabadiliko ya Katiba zote mbili, utengemano wa kijamii na utamaduni, kurasimisha juhudi za maridhiano na kuongoza mageuzi katika mafunzo ya maadili na malezi ya watoto.

Pia amesema ipo suala la uwajibikaji na utawala wa sheria, kusimamia mageuzi ya mifumo ya kisheria, uchaguzi, na haki za binadamu, kuleta mageuzi ya kikodi, pensheni na hifadhi ya jamii, pamoja na kilimo, uchumi na biashara kuelekea mwaka 2030 na kusimamia mageuzi katika huduma za habari na mawasiliano na Utafiti kwa Maendeleo.

Tunaomba kuwafikishia ujumbe wananchi wote wa Zanzibar kuyaamini kwa dhati maazimio muhimu yaliyomo katika Ilani yetu kama ramani ya matumaini yetu kwani wakati wa mabadiliko. Huu ni wakati wa ACT Wazalendo, kuleta mabadiliko hayo,” amesisitiza.

Othman amesema chama chao pamoja na kuzaliwa mwala 2014 lakini kilizaliwa upya mwaka 2019 baada ya kiongozi mtetezi wa Wazanzibari Maalim Seif Sharif Hamad na wafuasi waje kujiunga na ACT Wazalendo kufuatia jukwaa lao la mapambano ya kudai haki zao.

Amesema tokea wakati huo chama chao kiliandaa mikakati madhubuti ya kujipambanua kwa Watanzania na Wazanzibari.

”Miongoni mwa mikakati yetu ni ahadi ya chama kwa wananchi iliyofafanua maono mapana ya chama chetu ambapo miongoni mwa matunda hayo ni misingi iliyochavusha ilani yao ya mwaka 2025,”amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ilani hiyo ,Prof.Omar Fakih Hamad amesema kamati ilibeba jumla ya wajumbe 12 kutoka nafasi mbalimbali ambapo ilizinduliwa na kuanza kazi rasmi Mei 24,2025 na ilikamilisha kazi ya Msingi ya uandishi wa rasimu ya Ilani Agosti 2, 2025.

Amesema shughuli kuu katika uandaaji wa ilani hiyo iliweza kukusanya taarifa kutoka katika tafiti na nyaraka mbalimbali iiwemo REPOA,CAGs, SDGs na taasisi nyingine muhimu na waliweza kuchambua taarifa za awali na mapendekezo ya wajumbe na kuandaa vipaumbele, muundo na sura za Ilani.

Pia amesema wakiweza kuandaa dodoso fupi kwa makundi maalum ya jamii na sekta,kukusanya taarifa, mapendekezo, maoni, kutoka kwa wataalamu, wananchi na wadau wa kisekta,kuchambua data za utafiti na taarifa zingine kwa ajili ya kuchagua maeneo ya ilani pamoja na kuandaa muundo wa sura, masuala, malengo, sera na mikakati yachama katika Ilani.

Amesema ilani hiyo iliyozinduliwa ni kwa ajili ya uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 20202 na imeandikwa katika muundo wa sehemu tano, Sehemu ya Kwanza hadi Sehemu ya Tano pamoja na sehemu mbili ndogo.