JESHI la Polisi, Mkoa wa Pwani linamshikilia mkazi wa Mtaa wa Muhenza, Wilaya ya Kibaha, Rajabu Musa (23) kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi, Hamis Said maarufu kama ‘Mzee Mpili’ kwa tamaa ya kumiliki mali za baba yake, ikiwemo fedha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase alisema hayo juzi wakati akizungumza na vyombo vya habari mkoani hapo.
Alisema tukio hilo lilitokea Julai 11, mwaka huu majira ya saa sita usiku ambako Rajabu alimpiga baba yake kwa mateke na silaha nyingine za jadi.
Alieleza kuwa baada ya kuona baba yake amezidiwa alimburuza hadi eneo la shimo la choo na kumdumbukiza kwenye shimo hilo.
Kamanda Morcase alisema majirani walipoona ukimya umetawala baada ya kelele za vurugu walifika eneo la tukio na kufuata miburuzo na kumkuta mzee huyo akiwa amedumbukizwa kwenye shimo na kumkimbiza hospitali.
Alisema Julai 16, 2025 Mzee Mpili alifariki akiwa anaendelea kupatiwa matibabu. Kamanda Morcase pia, alisema licha ya mtuhumiwa kudaiwa kumuua baba yake kwa ajili ya mali pia inachangiwa na matumizi ya dawa za kulevya.
Naye mkazi wa Mtaa wa Muhenza, Joseph Lyimo alisema walimpeleka Mzee Mpili, Hospitali ya Tumbi na alipatiwa huduma ya kwanza na baadaye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili – Mloganzila ambako waliambiwa kuwa ana majereha kichwani hivyo ilihitajika Sh 200,000 kwa ajili ya matibabu zaidi.
Kwa upande wake, Mkazi wa Mtaa wa Muhenza, John Manda alisema walipofika eneo la tukio walimkuta Mzee Mpili akiwa anahangaika kwenye shimo hilo huku hali yake ikiwa mbaya.
“Tulipomtoa mtoto wake mkubwa alimuuliza baba nani amekudumbukiza humu Mzee Mpili alijibu kuwa ni Rajabu, alimuuliza zaidi ya mara mbili na akasema ni Rajabu ndio aliyefanya kitendo hicho,” alisema Manda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa huo, Moshi alisema wamesikitishwa na tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi na watoto kuepuka kufanya vitendo vya kihalifu.