Na Allan Kitwe, Tabora

JESHI la Polisi mkoani Tabora linamshikilia Hadija Jimmy Mrijo (39) mpare, kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa na watu wasiojulikana ili ajipatie fedha isivyo halali kutoka kwa mume wake.

Kamanda wa Polisi Mkoani hapa SACP Richard Abwao amethibitisha kushikiliwa mwanamke huyo ambaye ni mke wa Emanuel Peter Charles mkazi wa Tabora Mjini.

Amesema kuwa mtuhumiwa alikamatwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa mumewe kuwa alipigiwa simu na mtu asiyemfahamu akidai kuwa wamemteka hivyo awatumie fedha kiasi cha sh mil 2 ili wamwachie.

Amedokeza kuwa mume wa mtuhumiwa baada ya kupokea taarifa hiyo na kusikia mlio wa kuteswa aliingiwa na hofu na kuanza kutafuta kiasi hicho cha fedha ambapo alifanikiwa kutuma kiasi cha sh 1,385,800/-.

Kamanda Abwao amefafanua kuwa baada ya kufanya uchunguzi wa kina tumebaini kuwa mtuhumiwa hakuwa ametekwa ila alijiteka mwenyewe ili apate fedha hizo, akishirikiana na wenzake na wote wamekamatwa.

Ametaja watuhumiwa wengine waliokamatwa kuwa ni Ashura Hussein Salehe (48) mkulima, mnyamwezi (wifi wa Hadija) na Vitus Joseph (34) mkulima, muha aliyepiga simu kwa mume wa Hadija akidai kuwa wamemteka na wanataka hela.

Kamanda Abwao alieleza kuwa awali mtuhumiwa Hadija alidai kuwa ametekwa katika Kijiji cha Uyogo, Kata ya Kiemba, Tarafa ya Ulyankulu Wilayani Kaliua, wakati sio kweli, kwani alikuwa Kijiji cha Vumilia, Wilayani Urambo kwa ndugu.

Alibainisha kuwa Mkoa wa Tabora hauna vitendo vya utekaji hivyo akatoa wito kwa wananchi kuacha kutoa taarifa zinazoleta taharuki miongoni mwa jamii na kuwataka wanaofanyiwa vitendo vya ukatili kifamilia watoe taarifa ili zitatuliwe.

Aliwahakikishia kuwa Jeshi la Polisi Mkoani hapa limejipanga vizuri kudhibiti vitendo vya aina yoyote ile vinavyoenda kinyume na maadili ya jamii ili kukomesha tabia hizo.