Chama cha Alliance for Democracy Change (ADC) kimesema serikali yake itafuta misamaha ya kodi na kuondoa punguzo kwa bidhaa zote zinazoingizwa kutoka nje ya nchi wakati zinapatikana hapa nchini.

Ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2025-2030 imesema itapunguza uingizwaji wa bidhaa zinazozalishwa nchini kutoka nje ili kulinda soko la ndani kwa ajili ya bidhaa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya nyumbani.

Pia imesema itatoa ajira kwa wajasiriamali milioni 20 kila mwaka na itaanzisha benki kwa ajili ya kuwapatia vijana mikopo isiyo na masharti magumu au riba kubwa.

Imesema vijana watapunguziwa kodi kwa vifaa vinavyoingizwa nchini kwa ajili ya uzalishaji.

“Vijana watapewa ruzuku, mikopo nafuu kwa ajili ya ununuzi wa nyenzo za uzalishaji vikiwamo vifaa vya kazi, mahala pa kufanyia uzalishaji na biashara,’’ imesema.

Pia imesema itawapatia ruzuku ya uzalishaji wakulima, wavuvi, wafugaji, wazalishaji wa viwandani na wengine na itazuia usafirishaji wa malighafi za mazao nje ya nchi.

Kimesema kitaanzisha viwanda vitakavyozalisha bidhaa bora kutokana na malighafi za nchini vikiwamo vya kusindika majani ya chai badala ya kuuza chai ikiwa haijatengenezwa.

Vilevile serikali ya ADC itatoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana na kuanzisha viwanda vitakavyozalisha pembejeo, mbegu na vifaa vya kufanyia kazi.

Viwanda vingine ni vya kusindika bidhaa za tumbaku, matunda, kahawa, pamba, mazao ya baharini kama vile mwani, majongoo na samaki. Vingine ni viwanda vya kuchakata madini ili kutengeneza vito badala ya kuyauza madini ghafi.

Ilani imesema itarahisisha upatikanaji wa nishati ya maji na umeme, sambamba na ongezeko la matumizi ya nishati jadidifu ili kupunguza gharama za uzalishaji.