Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) kimeahidi kuanzisha mpango maalum wa ustawi wa jamii utakaompa kila mzazi fao la kumlea mtoto kuanzia anapozaliwa hadi kufikisha umri wa miaka 18, iwapo kitapewa ridhaa ya kuunda serikali baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Ahadi hiyo imetolewa leo Agosti 14,2025 na mgombea urais wa ADC, Wilson Elias Mulumbe, muda mfupi baada ya yeye na mgombea mwenza Shoka Khamis Juma, kuchukua fomu za kugombea urais katika Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma.

Mulumbe amesema mpango huo utapunguza mzigo wa malezi kwa familia na kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama na yenye fursa sawa.

Akifafanua zaidi, Mulumbe amesema Serikali yake pia itahakikisha elimu inatolewa bure kuanzia shule ya awali hadi vyuo vikuu, sambamba na kufutwa kwa makato ya elimu ya juu kwa wahitimu ili vijana waanze maisha ya kiuchumi bila kubebeshwa madeni.

Katika sekta ya afya, ameahidi matibabu bure kwa wananchi wote, kuanzia huduma za msingi hadi za rufaa, akisisitiza kuwa afya bora ni haki ya kila Mtanzania na si huduma ya anasa.

Aidha, huduma za umeme na maji amesema zitatolewa bure, huku wilaya zinazokabiliwa na uhaba wa maji zikipewa kipaumbele cha kupata maji safi na salama.

Kwa upande wa siasa, mgombea mwenza Shoka Khamis Juma amesema Serikali ya ADC itatoa ruzuku kwa kila chama cha siasa, kinyume na hali ilivyo sasa ambapo baadhi ya vyama havipati msaada wa kifedha.

Ameongeza kuwa sharti la sasa la kupata angalau asilimia 5 ya kura ili kunufaika na ruzuku litafutwa, ili kuhakikisha hata vyama vidogo vina nafasi ya kuimarika na kugombea.

Shoka pia amesisitiza kuwa ADC itaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kushirikisha vyama vyote katika kugawa rasilimali na kufanya maamuzi, akifananisha taifa na “keki inayopaswa kugawanywa kwa wote.”

Kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, amesema utaendelezwa na kuimarishwa, lakini baadhi ya maeneo yenye changamoto yatarekebishwa kwa maslahi ya pande zote mbili.

Wagombea hao wamehitimisha kwa kusisitiza kuwa katika serikali watakayoiunda, kila raia atalipa kodi kwa usawa, ili kuongeza mapato na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote bila ubaguzi.