Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kisarawe

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo amesema kauli ya Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Wakili Boniphace Mwabukusi kupinga jitihada za ACT Wazalendo kuhamasisha wananchi kulinda kura ina udhaifu wa kimantiki.

Ndugu Ado Shaibu ametoa kauli hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa ACT Wazalendo Jimbo la Kisarawe ulipfanyika leo tarehe 6 Julai 2025 Kisarawe Mjini.

“Nimefuatilia mjadala unaoendelea mtandaoni baada ya ACT Wazalendo kuzindua Operesheni Majimaji inayolenga kuwahamasisha Watanzania kulinda kura. Nimefarijika na maoni yote, yanayounga mkono na kupinga kampeni yetu. Sisi ACT Wazalendo tunafurahia mijadala na hatuna shida nayo” alisema Ndugu Ado Shaibu.

Hata hivyo Ndugu Ado Shaibu alisema kuwa baadhi ya hoja zinazotolewa zina udhaifu wa kimantiki ambao unapaswa kuweka bayana. Mathalani alisema hoja ya Rais wa Chama cha Wanasheria Tangamyika kusema kuwa kura zinapaswa kulindwa na sheria peke yake na kwamba wanaohamasisha kulinda kura kwa nguvu za umma kuwa matapeli ni hoja yenye udhaifu mkubwa wa kimantiki.

“Katika nchi za Kiafrika na zenye mifumo dhaifu ya kidemokrasia tunapaswa kuunganisha mapambano yote mawili, mapambano ya mifumo madhubuti ya kisheria na mapambano ya kuhamasisha nguvu ya umma dhidi ya mifumo kandamizi. Yeyote unayekuhamasisha kuacha chochote kati ya hivyo viwili au kutegemea kimoja pekee atakuwa anafanya makosa kwa kujua au kutojua. Sisi ACT Wazalendo tumeamua kwenda na vyote viwili, tutapigania mifumo madhubuti ya kisheria na tutahamasisha nguvu ya umma kulinda thamani ya kura” alisema Ndugu Ado Shaibu.