Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora imemhukumu kifungo cha miaka 30, Boniface Matale (30), mkulima na mkazi wa Kata ya Mbagwa wilayani humo, baada ya kupatikana na Hatia ya kumlawiti kijana mwenye matatizo ya akili kinyume na maumbile.

Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo Nasra Mkadamu ambapo ameeleza kuwa ametoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine.

Alifafanua kuwa mahakama imeridhika pasipo shaka na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo hivyo akatoa hukumu hiyo kwa mshtakiwa Boniface Matale ya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.

‘Adhabu hii ni fundisho kwake na kwa watu wengine wenye mazoea au nia ya kufanya vitendo vya namna hiyo, vitendo vya namna hiyo ni vya kikatili na havikubaliki miongoni mwa jamii’, alisema.

Nasra aliendelea kuimbia mahakama hiyo kuwa vitendo vya ukatili, ubakaji na ulawiti vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara Wilayani humo hivyo adhabu hizo zitakuwa ni fundisho Kwa wengine

Awali Wakili wa Serikali Enock Kigolya, aliiambia mahakama hiyo kuwa mnamo Agosti 19, 2025 majira ya usiku huko katika Kata ya Mbagwa nyumbani kwa kijana huyo, ambapo aliingia chumbani kwake na kumfanyia kitendo hicho.

Alidokeza kuwa kitendo hicho kilishuhudiwa na dada wa kijana huyo hivyo kufungua kesi hiyo namba 21407 ya mwaka 2025.

Awali mtuhumiwa huyo aliomba kupunguziwa adhabu kama atakutwa na hatia kwa kuwa ana umri mdogo na anatengemewa na wazazi wake

Licha ya ombi hilo mahakama ilitoa hukumu hiyo ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kumfanyia kitendo cha ukaliti mtu mwenye matatizo ya akili.