Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa ratiba ya uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi, udiwani wa kata/ wadi na viti maalumu kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Agosti 22 mwaka huu, Halmashuri Kuu ya chama hicho ya Taifa inatarajia kukaa kikao kufikiria na kufanya uteuzi wa mwisho wa majina ya wanachama wanaoomba nafasi ya ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo na viti maalumu.
Ratiba inaonesha Julai 28, mwaka huu Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa itakutana kufikiria na kuteua majina ya wana CCM wasiozidi watatu walioomba nafasi ya ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo na viti maalumu ili wakapigiwe kura za maoni.
CCM imetangaza Julai 30 kutakuwa na mikutano mikuu maalumu ya mikoa ya UWT kupiga kura ya maoni kwa wagombea wa ubunge wa viti maalumu (Tanzania Bara) na wagombea ubunge/ uwakilishi wa viti maalumu (Zanzibar) vya mikoa.
Mikutano mikuu ya kata/ wadi na jimbo itafanyika Agosti 4 kupiga kura za maoni za wagombea wa ubunge, ujumbe wa baraza la wawakilishi na udiwani wa kata/wadi (kwa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara).
Ratiba hiyo inaonesha kuanzia Julai 30 hadi Agosti 3, mwaka huu kutakuwa na mikutano ya kujitambulisha kwenye kata/wadi na jimbo kwa wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani kwa Zanzibar na Tanzania Bara.
Agosti 5, Kamati za siasa za kata/wadi zitawajadili wagombea udiwani na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati ya siasa ya jimbo/ wilaya na Agosti 6, Kamati ya siasa ya jimbo itawajadili wagombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa Wadi kwa upande wa Zanzibar na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati ya siasa ya wilaya.
Vikao vya Kamati za siasa za wilaya kujadili wagombea ubunge, ujumbe wa baraza la wawakilishi na udiwani na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati ya siasa ya mkoa vitafanyika Agosti 8, 2025.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa Agosti 13, vitafanyika vikao vya Halmashauri Kuu za CCM za mikoa kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani mmoja kwa kila kata/wadi iliyopo mkoani na udiwani wa viti maalumu.
Pia, Kikao cha Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kitapokea na kuchambua majina ya wagombea ubunge na ujumbe wa baraza la wawakilishi wa jimbo na viti maalumu kwa ajili ya mandalizi ya vikao vya uteuzi Agosti 16.
Agosti 19, Kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kitapokea na kuchambua majina ya wagombea ubunge na ujumbe wa baraza la wawakilishi wa jimbo na viti maalumu kwa ajili ya maandalizi ya vikao vya uteuzi.
Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa Agosti, 20 kitafikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya wanachama wanaoomba nafasi ya Ubunge na Ujumbe wa baraza la wawakilishi wa jimbo na viti maalumu.
Julai 19, 2025 Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alisema hatma ya uteuzi wa watiania walioomba kugombea nafasi za ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi viti maalumu na udiwani ndani ya CCM itajulikana Julai 28, 2025.
