Na Lookman Miraji

Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia katibu wake wa Halmashauri Kuu, itikadi, uenezi na mafunzo, Amos Makala kimetangaza ujio wa mkutano mkuu maalum wa CCM unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 na 30 ya mwezi Mei 2025.

Katika taarifa iliyotolewa leo Mei 17, 2025 na mwenezi Amos Makala imesema mkutano mkuu huo maalum utafanyika ukiwa umebeba ajenda kuu tatu muhimu zitakazojadiliwa katika mkutano huo.

Mkutano huo umebeba ajenda hizo tatu ambazo zitakuwa ni kupokea taarifa ya utekelezaji ya ilani ya chama cha mapinduzi kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020 mpaka 2025 taarifa zitakazowakilishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkutano mkuu huo pia utapokea na kuzindua rasmi ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2025 mpaka 2030 ikiwa ndiyo ilani itakayotumika na chama katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Pia mkutano mkuu huo utafanya kazi ya marekebisho madogo katika katiba ya CCM

Aidha mwenezi Makala ametoa rai kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kupitia tiketi ya chama cha mapinduzi watakaopitishwa kushiriki katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu kuhakikisha wanaisoma na kuielewa ilani ya chama itakayozinduliwa katika mkutano mkuu huo maalum.

Mkutano mkuu maalum wa chama cha mapinduzi utatanguliwa na kikao cha halmashauri kuu ya taifa kitakachofanyika Mei 28 jijini Dodoma kikao ambacho kitatanguliwa na kikao cha kamati kuu kitakachofanyika Mei 26 jijini Dodoma.