Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kampuni ya ALAF Limited, inayoongoza katika suluhisho mbalimbali za ujenzi, imejizatiti kuhakikisha inawajengea wanawake uwezo zaidi wa kushika nafasi za juu za uongozi  katika kampuni hiyo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya nne ya Mafunzo ya Wazawake katika Uongozi, kupitia program ya G for G (Girl for Girl) inayoendeshwa na ALAF hususani kwa wanawake, Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Bw.Lincoln Du Plessis alisema program hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwani miongoni mwa mambo mengine imewajengea wanawake wa ALAF kujiamini zaidi katika majukumu yao kazini.

Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Safal Group, Bi. Beatrice Imathiu (kushoto) akimkabidhi cheti Theresia Mmasy, mmoja wa wahitimu wa Mafunzo ya Wanawake na Uongozi ya Kampuni ya ALAF wakati wa mahafali yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja Maendeleo ya Vipaji wa Safal Group, Naomi Odongo.

Hata hivyo, aliwaasa wahitimu wa program hiyo kutambua kuwa uongozi ni uwajibikaji na sio nafasi tu anayopewa mtu. “Ni lazima muwe tayari kuwaongoza wengine ili nao wapate maarifa mliyoyapata nyinyi  na wapate ari ya kuwa viongozi wanaowajibika,” alisema.

Bw. Du Plessis pia aliwakumbusha wahitimu hao kuhusu kujiamini  na kuwa na mawazo chanya ili wawe viongozi bora katika kampuni ya ALAF.

“Hii ni kama safari ambayo ina milima na mabonde kwa hivyo lazima mujiandae kukabiliana na yote haya ili muwe viongozi bora.

Akifafanua kuhusu mafunzo hayo ya Wanawake na Uongozi, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa ALAF Limited, Bi. Hawa Bayumi alisema haya ni mahafali ya nne tangu kuanzishwa kwa programu hiyo ambayo imekuwa na manufaa makubwa mno kwa kampuni hiyo huku wanawake wengi zaidi wakipata nafasi za uongozi .

Afisa Mtendaji Mkuu wa ALAF Limited, Bibhu Nanda (kulia) akikabidhi zawadi kwa Pamela Mwanjali, ambaye ni mmoja wa wahitimu wa Mafunzo ya Wanawake na Uongozi ya ALAF Limited wakati wa mahafali yaliyofanyika Jijini Dares Salaam. Wengine kutoka kushoto ni Meneja Rasilimali watu wa ALAF Limited, Jumbe Onjero na Mkuu wa Uzalishaji wa Safal Group, Ashish Mistry.

“Leo hii wamehitimu wanawake 10 ambao wamepata mafunzo mbalimbali na maarifa ambayo yatawasaidia katika shughuli zao za kila siku hususani uongozi,” alisema.

Alieleza kuwa wahitimu hao, kutoka idara mbalimbali za ALAF, walipata vyeti baada ya kupitia mafunzo ya miezi kadhaa ya nadharia na vitendo hivi kuwajengea uwezo zaidi.

“Mimi mwenyewe ni matunda ya program hii na nilikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza kabisa kupata mafunzo haya na kuhitimu na sasa hivi nafurahi kuwa mmoja wa viongozi katika kampuni ya ALAF.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wote, Pamela Mwanjali ambaye ni Meneja Mauzo Kanda ya Pwani, alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa mno kwani wamehitimu wakiwa watu tofauti na mwanzoni kabla ya mafunzo hayo.

“Kwa niaba ya wenzangu, naishukuru sana ALAF kwa kutujengea uwezo huu na kutuamini kwamba tunaweza kushika nafasi za uongozi. Tumepikwa vizuri na sasa tunakwenda kutekeleza majukumu yetu vizuri zaidi kwa sababu tumejifunza mengi mno,” alisema.

Wahitimu wa Mafunzo wa Wanawake na Uongozi ya ALAF Limited wakiwa jkatika picha ya pamoja wakati wa mahafali yao Jijini Dar es Salaam.

Alitoa wito kwa makampuni mengine na mashirika yawajengee wanawake uwezo ili watambue kuwa na wao wanaweza kuwa viongozi.

ALAF, ambayo ilianza kufanya shughuli zake nchini Tanzania mwaka 1960, imekuja na suluhisho kamili kwa ajili ya shughuli za ujenzi ambazo hujumuisha bidhaa za kuekeza kwenye paa zilizopakwa rangi, Pamoja na bidhaa zingine kama yakiwemo mabomba aina mbalimbali yanayotumika kwenye shughuli za ujenzi.

www.alaf.co.tz

Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa ALAF Limited, Lincoln Du Plessis akizungumza wakati wa mahafali ya Mafunzo ya Wanawake na Uongozi ya ALAF Limited Jijini Dar es Salaam.